Featured

    Featured Posts

KANISA HALISI LINAVYOKIENZI KISWAHILI, IBADA ZAKE ZOTE NI KWA LUGHA HIYO TU HADI MAREKANI NA MATAIFA YOTE DUNIANI

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Kiswahili ni lugha ya Kibantu yenye misamiati mingi ya Kiarabu kwa asilimia 35 na ya Kiingereza asilimia10, inayozungumzwa katika eneo kubwa la Afrika ya Mashariki.

Kiswahili kilianza takribani miaka 800-1000 iliyopita katika mazingira ya vituo vya biashara vya pwani ambako wafanyabiashara kutoka Uarabuni, Uajemi na Uhindi walikutana na wenyeji Waafrika lakini lugha kuu ya kimataifa ya biashara hiyo ilikuwa Kiarabu.

Historia naeleza kuwa inaonekana lugha mpya ilijitokeza wakati wenyeji wa pwani, waliokuwa wasemaji wa lugha za Kibantu, walipopokea maneno mengi hasa ya Kiarabu katika mawasiliano yao. Kwa hiyo msingi wa Kiswahili ni sarufi na msamiati wa Kibantu pamoja na maneno mengi ya Kiarabu na inakadiriwa kuwa karibu theluthi moja ya maneno ya Kiswahili yana asili ya Kiarabu.

Kando ya Kiarabu toka zamani pia kuna athira ya lugha mbalimbali kama Kiajemi, Kihindi na Kireno.
Inaelezwa kuwa kuanzia karne ya 20 hadi sasa maneno mengi yamepokewa kutoka Kiingereza, na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Kifaransa, lakini pia kutoka lugha nyingine, hasa Kiarabu.

Kwa mujibu wa historia Kiswahili kilianza kuandikwa kwa herufi za Kiarabu pekee (سواحلي sawahili au لغة سواحيلية lugha sawahiliya), kwa karne nyingi.

Sarufi ya kwanza pamoja na kamusi iliandikwa mwaka 1848 na Dokta Ludwig Krapf huko Rabai Mpya/ Mombasa. Kiswahili kilikuwa na lahaja nyingi kutokana na lugha mbalimbali za Kibantu zilizochangia katika eneo husika.

Tangu karne ya 19 lugha ya Kiswahili ilianza kuenea barani kwa njia ya biashara. Wakati wa ukoloni wa Uingereza lugha ilisanifishwa na Kamati ya kimaeneo ya lugha ya Kiswahili kwenye msingi wa lahaja ya Unguja.

Inaelezwa kwamba hakuna hakika kuhusu idadi ya wasemaji wa lugha hiyo; idadi zinazotajwa zinatofautiana, lakini ni kati ya milioni 100 na 200, kwa sababu wasemaji wanaoitumia kama lugha ya kwanza hawapungui milioni 20, na wasemaji wanaoitumia kama lugha ya pili ni zaidi ya milioni 90.

Tena idadi ya wasemaji wa lugha ya kwanza inakua haraka, kwa sababu lugha inaenea katika maeneo ambapo hapo awali lugha nyingine zilitawala; hasa katika miji ya Tanzania imekuwa lugha kuu, badala ya lugha za kikabila.

Kutokana na mchanganyiko wa watu hata ndani ya nyumba moja, kama vile wanapooana watu wa makabila tofauti, jambo ambalo limekuwa la kawaida hasa Tanzania, ambayo inaongoza kwa matumizi ya Kiswahili. Kwa watoto wengi kimekuwa lugha mama.

Mbali na Tanzania nchi nyingine ambako Kiswahilo kinazungumzwa ni Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Somalia, Zambia, Malawi na visiwa vya Bahari Hindi kama Visiwa vya Ngazija (Komoro).

Kiswahili kimekuwa lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika Tanzania ni lugha ya taifa; ni lugha ya shule za msingi, lugha ya utawala serikalini na mahakamani; inatumika kote nchini, makanisani, misikitini, redioni, kwenye runinga na idadi kubwa ya magazeti.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada za kukiendeleza Kiswahili kwa sababu ni lugha ya taifa. Sera ya elimu ya mwaka 2015 imechagua Kiswahili katika miaka 10 ijayo kiwe lugha ya kufundishia katika ngazi zote, ikiwemo ile ya chuo kikuu, ingawa utekelezaji wake umesimama.

Kenya:
Kenya Kiswahili ni lugha ya taifa tena lugha rasmi, sawa na Kiingereza, baada ya rasimu ya katiba mpya kupitishwa Agosti 4, 2010; Kiswahili ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kati ya wananchi wakikutana nje ya eneo lenye kabila moja tu.

Nchini hu,o ni lugha inayofundishwa lakini si lugha ya kufundisha mashuleni; ni lugha inayotumika na polisi na jeshi, ni lugha ya kuhutubia wananchi mjini na kitaifa; sehemu za ibada makanisani zinatumia Kiswahili; kuna gazeti moja tu la Kiswahili; sehemu za programu redioni na kwenye runinga ni kwa Kiswahili. Hata hivyo, lugha inachanganywa mara nyingi na Kiingereza na lugha za maeneo au za kikabila.

Uganda:
Kimetangazwa Kiswahili kuwa lugha ya taifa tangu 2005; iliwahi kuwa lugha ya taifa wakati wa utawala wa Idi Amin; wakati wa ukoloni ilifundishwa mashuleni ikaelekea kuwa lugha rasmi pamoja na Kiingereza lakini matumizi haya yalipingwa hasa na Waganda hivyo Waingereza waliacha mipango hiyo.

Ni lugha ya polisi na jeshi, hali ambayo imeleta ugumu kwa lugha kukubalika na wananchi wengi kutokana na historia ya utawala wa kijeshi Uganda; watu wengi bado hukumbuka hasa matusi ya wanajeshi waliowatesa wakisema Kiswahili. Lakini kuna maeneo ya Uganda ambako Kiswahili kinatumiwa na watu wengi kama lugha ya sokoni na barabarani. Wona UBC, WBS tv. Mwaka 2005 bunge lilipiga kura kukifanya lugha rasmi ya pili kwa kuwa kinazungumzwa zaidi (nje ya Buganda).

Rwanda:
Februari 8, 2017 bunge lilifanya Kiswahili lugha rasmi ya nne baada ya Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza nako Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Kiswahili ni kati ya lugha nne za kitaifa (pamoja na Kilingala, Kiluba na Kikongo), pia lugha ya jeshi. Kiswahili kilifika mashariki ya nchi na misafara ya biashara ya watumwa na pembe za ndovu kutoka Zanzibar na pwani ya Tanganyika. Imeenea zaidi kati ya mchanganyiko wa wafanyakazi kwenye migodi ya Shaba.

Kiasili Kiswahili kilikuwa lugha ya kwanza tu ya wakazi wa miji ya Waswahili kwenye pwani, katika sehemu za pwani pia kijijini. Baada ya kuenea kimekuwa lugha ya watu wengi mjini hasa Tanzania lakini pia Kenya.
kimeenea zaidi kama lugha ya mawasiliano na biashara pale ambako watu wa makabila mbalimbali wanakutana. Pamoja na nchi zinazotajwa hapo juu Kiswahili kinatumika Kaskazini mwa Msumbiji, Kusini kabisa ya Somalia, Mashariki mwa Burundi.

Maeneo ya mpaka wa Tanzania kuna pia wasemaji kadhaa huko Malawi na Zambia.
Tanzania na Kenya zilipokea wakimbizi wengi waliojifunza Kiswahili lakini hakuna uhakika kama bado kinatumiwa nao baada ya kurudi Afrika Kusini, Rwanda, Sudan Kusini, Somalia n.k.

Lugha ya Kiswahili imekuwa na umuhimu mkubwa duniani kwa jumla, na hasa Afrika, kwa sababu ya kuenea kwake nchi mbali mbali, na kukusanya kwake watu wa makabila na nchi kadha wa kadha wakaweza kufahamiana kwa lugha moja, hasa ilivyokuwa ni lugha mojawapo katika lugha kubwa za Afrika ambazo zinachukuwa mahala pa lugha za kigeni na wakoloni, kama Kiarabu, Kiurdu, Kiebrania, Kireno na kadhalika.

Hali ya kukua Kiswahili Kimataifa imedhihirika pia kwa kuwa imekuwa inatumiwa katika kusambaza habari katika vituo mbalimbali ulimwenguni kama vile Sauti ya Amerika, BBC, Deutsche Welle, Monte Carlo, RFI, na nchi nyinginezo kama vile Uchina, Urusi, Irani. Aidha, imekuwa ni mojawapo ya lugha muhimu zinazofundishwa katika vyuo vikuu nchini Marekani, Uingereza, Ulaya bara, Urusi, Uchina, na barani Afrika.

Mwaka 2018 Afrika Kusini ilikubali Kiswahili iweze kufundisha shuleni kama somo la hiari kuanzia mwaka 2020. Botswana ilifuata mwaka 2020, na Namibia ina mpango kama huo. Pia Ethiopia na Sudan Kusini zimeanza kufundisha Kiswahili.

Mojawapo ya juhudi za Serikali kukuza Kiswahili ni kuwepo kwa taasisi zinazolenga kukikuza na kuimarisha kama vile Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na idara za Kiswahili katika vyuo vikuu vingine vya Kenya na pia Uganda.

Nchini Tanzania kuna Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ilhali nchini Kenya kuna Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). BAKITA na CHAKITA pamoja na wawakilishi kutoka Uganda wanaandaa kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki (BAKAMA).

Uchunguzi wa Kiswahili huendelea pia katika idara za vyuo vikuu vingi duniani, kwa mfano katika Institute National des Langues et Civilisations Orientales, jijini Paris, Ufaransa.
Kamusi za Kiswahili

    Faida za kutumia lugha ya Kiswahili zinatajwa kama ifuatavyo:
    1. Husaidia kuleta umoja wa bara zima.
    2. Hudumisha utamaduni wa Kiafrika kuliko kufuata kasumba.
    3. Hufanya Waafrika waamini zaidi mambo yao kuliko kutegemea tu ya kigeni.
    4. Hurahisisha mawasiliano baina ya watu wa Afrika Mashariki.
    5. Husaidia kuwa na mahusiano ya kibiashara na watu mbalimbali.
    6. Ni ishara ya kuwa huru na kushikamana.
    7. Ni utambulisho wa jamii husika (utaifa).
    8. Husaidia kukuza na kuendeleza sanaa.
    9. Husaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika taifa husika.
    10. Husaidia kupata ajira katika vyuo na shule mbalimbali zinazofundisha lugha ya Kiswahili hata nje ya nchi.
    11. Husaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wa lugha hiyo watakaofanya vizuri katika masomo kwa kuyaelewa zaidi.
    12. Husaidia kuikuza na kuieneza ndani na nje ya jamii.

KANISA HALISI LINAVYOKIENZI KISWAHILI
Natamani kukieleza Kiswahili kwa kina, lakini nahofia nisikuchoshe, hivyo nimejaribu kuandika hayo machache ili nipate fursa ya kukuandikia kuhusu Kanisa ambalo katika kukienzi Kiswahili hueendesha Ibada zake zote kwa Kiswahili tu katika vituo vyake vyote ndani ya Tanzania na mataifa ya nje ikiwemo Ujerumani na Marekani.

Bila shaka kwa jinsi hiyo ni sifa kubwa sana kwa Kanisa kukithamini na kukienzi Kiswahili, maana licha Kiswahili kutapakaa Duniani na nchini Tanzania kuwa Lugha ya Taifa, lakini bado kuna nyumba nyingi za Ibada tena Tanzanaia ambazo waendesha ibada huwa hawawezi kuziendesha kwa Kiswahili peke yake (hapo siwalaumu ni mfano tu).

Kanisa nilalozungumzia kuhusu kustahili sifa kwa kukienzi Kiswahili, ni Kanisa linaloitwa Kanisa Halisi, ambalo Makao yake Makuu yapo eneo la Tegeta Namanga Jijini Dar es Salaam.

Kanisa hili, mbali na kutumia Kiswahili katika kuendesha Ibada zake Duniani kote, lakini pia linakitumia Kiswahili kwa maneno mengi yaliyoshiba staha; baadhi ya maneno ambayo nimewahi kuyasikia  yakitamkwa kwenye mazungumzo na kwenye Ibada za Kanisa hilo, ni Kama, badala ya kusema Mungu wanasema CHANZO HALISI.

Baadhi ya maneno mengine ni Uzao badala ya Waumini, Kao Kuu badala ya tulivyozoea kusema Makao Makuu, kushiriki badala ya neno kula, sehenu ya usafi badala ya neno choo, Matengenezo badala ya neno Hospitali, Hongera badala ya neno pole na matunda badala ya neno sadaka.

Sasa hapo bila shaka utauliza kwa nini Kanisa Halisi wameshikilia Kiswahili na kukienzi kwa kiwango hicho. Jibu nililonalo (siyo la Kanisa Halisi wenyewe), ni kwamba Wanakienzi Kiswahili kwa kuwa ndiyo lugha lenye usiano wa karibu na chimbuko la Kanisa hilo maana ndilo Kanisa pekee liloanzia Tanzania, mkoani Kigoma.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi ndani na Nje ya Tanzania ambaye jina lake rasmi ni Baba Halisi, anasema Kanisa hilo lilianzia Tanzania baada ya majira ya waliotumwa wote kufikia ukomo, akifafanua kuwa waliotumwa ni Moyo wa Mwanzo (Mwa.1:1/ Mith.3:16), Kerubi (Eze. 28:16) Adamu wa Kwanza ( Mwa.2:16),  Musa (kut.3:10), Eliya Mtishbi (1 Fal. 17:1), Yesu (Mdo.10:38), Agamu wa Pili (1. Kor.44:49), Miaka 1000 (Isa. 33:6) na Nafsi ya Kwanza (1 Yoh.5:8).

Anasema Ufahamu unaofundishwa na Kanisa Halisi unatokana na Sauti iliyosikika Tanzania mkoani Kigoma, mwaka 2015, Mwaka 2019 na mwaka 2020, na kwamba ufahamu huo ulishaandikwa na kitabu chake kilizinduliwa mkoani Arusha, Kitabu chenye kinaitwa Ufahamu ulioanzia Tanzania kwenda Mataifa mengine.

Baba Halisi anafafanua zaidi kwamba Kanisa Halisi ni tofauti kabisa la Siloamu kama ambavyo wengi hudhani, kwa sababu Waliotumwa wote ndiyo waliokuwa Siloamu (Yohana 9:7) na kwamba ni Kanisa Halisi tu ndiyo ambalo siyo Siloamu kwa kuwa limeanza baada ya Majira ya Waliotumwa kufika ukomo yaani 2017.

Baba Halisi akiwa na Kitabu cha Ufahamu Ulioanzia Tanzania kwenda Mataifa Mengine
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana