Na Bashir Nkoromo, Blog ya Taifa ya CCM, JNICC
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.
Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina tangu wakati huo hadi sasa ni Kumiliki/Kutunza, Kushauri na kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika kampuni na Mashirika ya Umma au Taasisi ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya Umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya Sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Ofisi inayojitegemea kimuundo na pia katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) Ofisi ilikabidhiwa majukumu ya Shirika hilo.
Chini ya Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu, Ofisi hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya Umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ofisi hiyo ya Msajili wa Hazina chini ya uongozi mahiri wa Mchechu na safu yake ya utendaji imekuwa ikipambana kuhakikisha wakati wote inasimamia kwaa umahiri na weledi mkubwa kuhakikisha mashirika na kampuni nchini zinatoa huduma bora kwa zile zinazotoa huduma tu na kuhakikisha zile za uzalishaji zinatoa faida yenye tija.
Ofisi hiyo mbali na kusimamia imekuwa ikiishauri serikali kufanya mambo mbalimbali au kuchukua hatua kadhaa katika kuboresha mashirika na kampuni hizo, katika maeneo mbalimbali ikiwemo sheria na taratibu pale Ofisi hiyo inapojiridhirisha kuwa hatua zinapaswa kufanyika.
Kwa mujibu wa Mchechu, hadi sasa kuna jumla ya Kampuni na Mashirika auTaasisi 298 za Umma, ambapo 248 ni Taasisi, Mashirika ya Umma, na Wakala wa Serikali na 50 ni Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.
“Kampuni zote ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache ni za Kibishara ambapo 40 ziko ndani ya nchi na 10 ziko nje ya nchi. Aidha Taasisi, Mashirika ya Umma, na Wakala wa Serikali 213 ni za utoaji huduma huku 35 ndio za kibishara", akasema Mchechu.
Akizungumza katika kikao kazi baina yake na Wahariri wa Vyombo vya Habari sanjari na Waandishi a habari, kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, jana, Mchechu alieleza mambo kadhaa ikiwemo Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma.
Mchechu akasema, Muswada huo utakapokuwa sheria, sheria hiyo italeta mageuzi makubwa ya kiutendaji kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina na mabadiliko ya Utendaji (Reforms) ambayo yataongeza tija na mafanikio katika utendaji kazi wa Kampuni na Mashirika au taasisi za Umma.
Akasema kimsingi Kampuni au taasisi ni wazalishaji na zinapaswa kuzalisha kwa ajili kugharamia mipango yao binafsi na ya serikali pia na kubainisha kuwa hadi sasa kuna baadhi ya Mashirika yanafanya vizuri na mengine hayafanyi vizuri na kwamba hapo Msajili huangalia ni kwa nini mengine yanafanya vizuri na kwa nini mengine hayafanyi vizuri ili kuchukua hatua.
Ni kweli Msajili wa Hazina amekuwa akichukua hatua kwa yake yasiyofanya vizuri ikiwemo kubadilisha uongozi au kuyafuta, lakini inaonekana pamoja na kuchukua hatua bado upo ubabaifu wa baadhi ya kampuni na mashirika ya umma, sasa ikiwa ni hivyo ni dhahiri kuna ulegevu fulani kwenye sheria hivyo uhitaji wa kuwepo sheria iliyoboreshwa ni muhimu.
Kulingana na Mchechu moja ya mambo ambayo yanachochea umuhmu wa sheria mpya ni Jina la sasa la Ofisi ya Msajili wa Hazina ambalo lina mkanganyiko fulani, maana inaonekana kama ni ofisi ya kusajili tu wakati majukumu yake ni zaidi ya hapo ikiwemo kusimamia uwekezaji, hivyo mabadiliko ya sheria yataendana pia na Ofisi ya Msajili wa Hazina kubadili Jina hilo na kuitwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investments Authority – PIA).
Mchechu anasema pamoja na kubadili jina, katika muundo ndani ya mabadiliko ya sheria Ofisi ya Msajili wa Hazina wakati itakapokuwa PIA, itaanzisha Mfuko wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Fund -PIF), ambao kazi yake itakuwa kuzisaidia Taasisi kuimarisha mitaji na kufafanua tofauti ya Mfuko huo ni kwamba wenyewe siyo Mfuko wa Jamii au Mifuko kama ile ya Kilimo.
Kuhusu umuhimu wa ujio wa Mfuko huo wa PIF, Mchechu anasema mojawapo utapanua wingo kuliko uliopo sasa ambao ni mfinyu. "Katika hali ya sasa OTR inawajibika kusimamia utendaji wa Taasisi zote za umma, imepewa mamlaka ya kuwekeza katika Taasisi na kusimamia uwekezaji, lakini wigo ni mfinyu", akasema.
“Katika mapendekezo ya muundo mpya, Ofisi ya Msajili wa Hazina sasa itakuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investment Authority - PIA) lengo ni kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa duniani.” Alisema.
Lakini pia katika Sheria mpya yatakuwepo mabadiliko ya namna ya kuajiri Watendaji Wakuu kwenye Kampuni na Mashirika au taasisi za umma, ambapo badala ya mfumo wa sasa, watakuwa wakiajiriwa kwa mikataba ya muda mfupi ya miaka miwili tu, ili wasiofaa waondokea bila kuendelea kudai maslahi zaidi na wanaofaa wapewe mikataba mipya.
Kwa jumla Mchechu anasema ili kuongeza ufanisi katika Kampuni na Mashirika au taasisi hizo mambo manne lazima yazingatiwe ambayo akayataja kuwa ni (i) Kuwa na uongzi bora (Good Leadership), (ii)Taasisi kutoingiliwa (kuwa huru), (iii) Kuwa na Rasilimali za kutosha (Resources) na (iv) Kupima utendaji (KPI).
Mchechu akatolea mfano kuhusu kupima utendaji, akasema "tumetengeneza vigezo vipya, zamani kulikuwa na vigezo ambavyo havijazingatia sekta. Unapomsimamia Tanesco au Muhimbili hawa kazi ni tofauti na hadi vigezo vyao, hivyo ni lazima vigezo viendane na sekta husika na asili ya taasisi inavyofanya kazi yake.”
Akarejea kauli yake kuwa ili kuleta tija mabadiliko katika taasisi za umma hayaepupikiki akawataka watendaji kujipanga na kuwa tayari kwa mabadiliko hayo ambayo tayari yameanza.
“Tumeshaanza, mabadiliko mtaona tunachanganya damu changa na wale wakongwe, na inapobidi tunachukua mtendaji kutoka sekta binafsi kuja kuongoza taasisi ya umma. Ofisi yetu inashughulika na Watendaji na Wenyeviti wa Bodi, hawa ni watu wazito, hivyo najua kazi itakuwa ngumu lakini lazima mabadiliko yafanyike", akasema Mchechu.
Akasisitiza "Mtarajio ya Mhe, Rais ni kuona taasisi hususan zile za kibiashara zinatengeneza faida zitakazozalishwa na kuingizwa Serikalini au kujiendesha pasipo utegemezi wa Serikali kuu, hivyo ni lazima kuwepo mabadiliko ili kuongeza tija na ufanisi."

Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akizungumza katika Kikao Kazi chake na Wahariri wa Habari, kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, jana Novemba 28, 2023.
Tafadhali soma Wasilisho hili👇 alilotoa Mchechu.























Post a Comment