Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiomba Serikali ya Japan ikubali kutoa mafunzo zaidi kwa Madaktari Bingwa wa upasuaji (Nephrologist Surgeon Specialist) na Madaktari Bingwa (Nephrologist Physician Specialist) wa magonjwa ya figo na moyo kutoka Tanzania ili kukidhi mahitaji makubwa ya madaktari hao nchini.
Waziri Mkuu amewasilisha ombi hilo jana jioni (Septemba, 02, 2019) wakati alipozungumza na Mshauri Maalum wa Masuala ya Afya wa Taasisi ya Tokushukai General Incorporated Association iliyo chini ya Serikali ya Japan, Bw. Akio Egawa kwenye uwanja wa ndege wa Narita nchini Japan akiwa njiani kurejea nyumbani.
Waziri Mkuu alisema hivi sasa Tanzania ni kimbilio kwa nchi jirani katika tiba ya moyo na figo, hivyo Madaktari Bingwa wa Upasuaji na Madaktari Bingwa wa magonjwa hayo wanahitajika sana.
Alisema baada ya hospitali ya Benjamini Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kufanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa saba chini ya ufadhili wa Taasisi hiyo, nchi jirani pia zinategemea kupata huduma hiyo nchini Tanzania, hivyo madaktari na vifaa tiba zaidi vinahitajika Ili kujenga uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wa ndani na nje.
Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Japan kupitia Taasisi hiyo kwa misaada yake ambayo kwa kiwango kikubwa imefanikisha kuanzishwa kwa tiba ya upandikizaji figo katika hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Nashauri uandaliwe utaratibu wa kubadilishana watalaam ili Watanzania waende Japan kutibu wagonjwa na Wajapan waje nchini kufanya kazi kwenye hospitali zetu lengo likiwa ni kubadilishana ujuzi na kuongeza uzoefu.”
Pia, Waziri Mkuu alimkaribisha nchini Tanzania Bw. Egawa ili aweze kuona mwenyewe maeneo mengine ambayo Taasisi anayoiongoza inaweza kusaidia ili kuifanya nchi yetu kuwa na uwezo mkubwa katika tiba ya uapandikizaji wa figo Barani Afrika.
Waziri Mkuu alisema amefurahi kufahamu kuwa Bw. Egawa ameishi Tanzania kwa miaka mitatu akifanya kazi kwenye ubalozi wa Japan uliopo Dar es Salaam, hivyo anaifahamu vizuri Tanzania na anajua umuhimu na mahitaji ya huduma za afya nchini na anafahamu mikakati Serikali kuhusu kuboresha huduma za afya.
Kwa upande wake, Bw. Egawa alimwahidi Waziri Mkuu kuwa Taasisi yake iko tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuendelea kusaidia hospitali ya Benjamin Mkapa ili kuiimarisha na kuiwezesha kufanya vizuri zaidi katika huduma ya tiba ya figo na moyo. Alisema taasisi yake iko tayari kuendelea kutoa ushirikiano na Serikali ya Tanzania.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, SEPTEMBA 03, 2019.
Post a Comment