MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti amewashukia vikali baadhi ya wanasiasa Wilayani Simanjiro wanaowagawa wananchi katika makundi ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa tiketi ya CCM ili wapate nafasi ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa ubunge 2020.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Manyara Mnyeti aliyasema hayo jana katika kijiji cha Narakauo Kata ya Loiborsiret kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano wilayani Simanjiro.
"Mwisho wa wanasiasa uchwara wa wilaya ya Simanjiro wanaotumia nafasi ya makundi na kugawa wananchi ili wapite katikati yao na kupata ubunge imefika mwishoni," alisema Mnyeti.
Alisema anataka kuona Simanjiro mpya moja yenye wananchi wenye kutaka maendeleo na siyo kugawanywa na baadhi ya wanasiasa uchwara wanaogawa wananchi kwa maslahi yao ya kutaka kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Alisema yeye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa ndiyo sababu wakafuta mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ndani ya CCM wilayani Simanjiro na kuagiza uanze upya kwa lengo la kuondokana na ubabaishaji.
"Wananchi wa wilaya ya Simanjiro hivi sasa wanataka maendeleo hawahitaji tena siasa uchwara zisizo na muelekeo wenye manufaa kwao kwa kutumia nafasi ya uchaguzi wa serikali za mitaa," alisema Mnyeti.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula aliwataka wananchi wa eneo hilo kutowachagua viongozi wanaojihusisha na uuzaji wa ardhi ili kuepusha migogoro ya ardhi.
Mhandisi Chaula aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kutumia nafasi hiyo vizuri ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwaondoa madalali wa kuuza ardhi na kuondokana na migogoro ya ardhi.
"Mkitumia makosa kwa kuchagua madalali wa ardhi baadaye msije ofisini kwangu kunisumbua kwani mtakuwa mmewachagua wenyewe na vijana wa sasa wanasema itakula kwenu," alisema mhandisi Chaula.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizindua madarasa matatu ya shule ya msingi Loong'swani kata ya Terrat Wilayani Simanjiro.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa Kata ya Terrat kwenye ziara yake ya siku tano wilayani Simanjiro jana.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti (wapili kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula (kushoto) wakipiga makofi baada ya kukagua nyumba ya kisasa ya mfugaji wa kijiji cha Narakauo Isaya Mongele, kulia ni Diwani wa Kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga Mardadi.
Post a Comment