Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kwa kuwachapa viboko wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya kwa madai ya kuhusika kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo.
“Leo nimeongea na Mkuu wa mkoa wa Mbeya na kumpongeza kwa kuwachapa wale wanafunzi viboko, yaani serikali inatoa fedha inajenga madarasa halafu hao wanafunzi wanayachoma, nimeagiza wale wanafunzi kidato cha tano na sita wote wafukuzwe na bodi ya shule ivunjwe” Amesema Rais Magufuli
Rais Magufuli ameyasema hayo leo katika ziara yake mkoani Songwe ambapo amesema viboko vinafundisha na kuwa ipo haja ya kufanyia marekebisho sheria inayozuia adhabu hiyo.
Amesema siku wanafunzi hao wakirejea shuleni lazima wazazi wao walipe fedha hizo kwa ajili ya kukarabati mabweni.
“Na wale wengine waliohusika kabisa peleka jela. Ndugu zangu nasema haya sio kwamba sina huruma nina upendo mkubwa na nimekuwa mwalimu nafahamu,” amesema Rais Magufuli.
Jana Oktoba 3, 2019 Chalamila aliwachapa viboko wanafunzi hao kwa madai ya kuhusika kuchoma moto mabweni mawili ya shule yao, leo asubuhi Oktoba 4, 2019 akaagiza wanafunzi wa kidato cha tano na sita warudishwe nyumbani hadi Oktoba 28, 2019
Post a Comment