Chanjo hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya Marekani ya Merck & CO tayari imeshaanza kutumika ili kujaribu kuwakinga watu dhidi ya mlipuko hatari wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Dakta Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuwa, chanjo hiyo tayari imeokoa maisha ya watu wengi katika mlipuko wa sasa wa Ebola.
Mlipuko wa homa hatari ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umeuwa watu zaidi ya 2,100 tangu katikati ya mwaka jana. Huu ni mlipuko wa pili mkubwa kuiathiri Kongo katika historia baada ya maradhi hayo kuziathiri nchi za magharibi mwa Afrika mnamo mwaka 2013 hadi 2016 na kuuwa watu zaidi ya 11,300.
Chanjo hiyo ya Merck ambayo kampuni zalishi imeipa jina la kibiashara la "Ervebo" inatarajiwa kupata leseni kamili ya uuzaji kutoka Kamisheni ya Ulaya katika wiki chache zijazo.
Post a Comment