Charles James, Michuzi TV
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amesema jumla ya wananchi waliochukua fomu za kugombea uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini walikuwa 555,036 na waliorejesha 539,993 sawa na asilimia 97.29 na asilimia 2.7 hawakurejesha kwasababu mbalimbali
Mhe Jafo amesema zaidi ya rufaa 13,500 zimewasilishwa na vyama vya siasa kwenye kamati za rufaa za uchaguzi wa serikali za mitaa.
Amesema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo jina la mgombea likiteuliwa linabaki kwenye katarasi za kupigia kura hata kama amejiengua kushiriki.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na wandishi wa habari ambapo amesema vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo vilipeleka rufaa zao kwenye Kamati za maeneo yao
Amesema vyama vyote vimewasilisha rufaa zao ikiwemo Chama cha Mapinduzi, CUF, ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi ambapo rufaa zilizowasilishwa ni 13,500 na kusema Kamati zinaendelea kufanya maamuzi na tayari zingine zishatoa majibu ya rufaa na kesho watatoa hali halisi ya mchakato mzima wa uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.
" Baada ya mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu kukamilika, kulikuwa na nafasi ya kushughulikia mapingamizi mbalimbali ambayo yamewasilishwa kwenye kamati za rufaa za maeneo husika ambapo mwisho wa kupitia rufaa hizo ni leo.
Kuna ngazi za mapingamizi na jambo hili ni la kidemokrasia huwa linafanyika, ibara ya 23 ya kanuni zetu inasema kamati za rufaa zina majukumu ya kupitia rufaa zote zinazojitokeza,”amesema.
Aidha amesema katika ziara yake aliyoifanya mikoa mbalimbali kukagua shughuli zinazofanywa na kamati za rufaa kwenye mikoa mbalimbali Singida, Dodoma, Manyara, Iringa na Njombe alipitia baadhi ya fomu zilizokuwa zimepitiwa na kamati hizo na kubaini kuna makosa kwenye ujazaji fomu.
“Kama vile mtu ameandika umri amezaliwa mwaka 2019, sehemu zingine mtu ameandika hata halmashauri yenyewe haiitwi hiyo msaidizi wa uchaguzi afanye nini?, mwingine sehemu ya saini ameweka tarehe halafu sehemu ya tarehe ameweka saini, fomu zingine mtu amejidhamini mwenyewe, wasimamizi walifanya kazi yao kwa mujibu wa kanuni,”amesema.
Ametaja mapungufu mengine ni kutofautiana majina kwenye fomu na daftari la wapiga kura wa uchaguzi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma kuhusiana na mchakato mzima wa uchukuaji na urejeshaji fomu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.
Post a Comment