Jeshi la Mali limetangaza kuwa, wanajeshi wake 53 na raia mmoja wameuawa katika hujuma iliyofanywa na kundi la watu waliokuwa na silaha dhidi ya kambi moja ya jeshi kaskazini mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Mali imesema kuwa, shambulizi hilo la kigaidi limefanyika katika eneo la Indelimane mkoa wa Menaka ulioko kaskazini mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Mali na Niger.
Waziri wa Habari wa Mali, Yaya Sangare amesema hali ya mambo imedhibitiwa na kwamba kazi ya kutambua miili ya askari waliouawa katika hujuma hiyo ya kigaidi inaendelea.
Hujuma hiyo inahesabiwa kuwa miongoni mwa mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Mali katika miezi ya hivi karibuni. Serikali ya Bamako imetangaza kuwa jeshi la ziada limetuma katika eneo hilo kutuliza hali ya mambo na kuwasaka magaidi waliohusika na hujuma hiyo.
Shambulizi hilo limefanyika mwezi mmoja baada ya kundi moja la kigaidi kuua wanajeshi 40 wa Mali katika mpaka wa nchi hiyo na Burkina Faso.
Hadi sasa hakuna kundi lililotangza kuhusika na hujuma hiyo.
Post a Comment