Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania leo amemteua Charles Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na hivyo kuchukua nafasi ya Profesa Mussa Assad ambaye kipindi chake kinamalizika.
Kwa mujibu wa taarifa, Kichere aliwahi kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapatano Tanzania (TRA) kabla ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Magufuli.
Taarifa ya uteuzi huo imesomwa leo na Balozi John Kijazi ambaye amesema kipindi cha uongozi cha miaka mitano cha Profesa Assad kinaisha kesho.
Mapema mwaka huu kuliibuka mgogoro baina ya Profesa Assad na Bunge la Muungano ambapo alionya kuwa mgogoro huo ungeibua mgogoro wa kikatiba Tanzania. Mwezi Aprili Bunge la Tanzania lilipitisha azimio la kutofanya kazi na CAG Assad baada ya kumtia hatiani kwa tuhuma za kudharau chombo hicho.
Mgororo huo ulianza Disemba 2018 baada ya CAG Assad kuiambia Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.
Spika Job Ndugai alilieleza Bunge mwezi Januari kuwa maelezo ya Assad yalioonesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo.
Post a Comment