Featured

    Featured Posts

WATOTO WAWASHIWA VIFAA VYA KUWASAIDIA KUSIKIA


 Bi. Maria Mosi akionyesha uso wa furaha wakati mtoto wake Gloria Raphael mwenye umri wa miaka mitatu kuanza kusikia sauti kwa mara ya kwanza baada ya kuwashiwa kifaa cha usikivu alichopandikiziwa kwa ajili ya kumsaidia kusikia
 Mtoto Ethan Riziki mwenye umri wa miaka saba akilia baada ya kusikia sauti kwa mara ya kwanza.
Mtaalam wa huduma ya usikivu Muhimbili Bw. Mathayo Majogoro (kulia) akirekebisha sauti kifaa cha usikivu kwa mtoto Uebert Kigala mwenye umri wa miaka saba na nusu.
 Daktari Bingwa wa Upasuaji Masikio, Pua na Koo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Dkt. Godlove Mfuko (katikati) akizungumzia zoezi la uwashwaji wa vifaa vya usikivu (Switch on) kwa watoto wawili waliopandikizwa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlear Implant) mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu, kushoto ni Dkt. Aveline Kahinga na kulia ni Dkt. John Masago.
 Mtaalam wa Sauti Bw. Fayaz Jaffer akielezea namna vifaa vya usikivu vinavyofanya kazi.


Watoto wawili wawashiwa vifaa vya kusaidia kusikia
Watoto wawili ambao wamewekewa vifaa vya kusaidia kusikia katika hospiali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila leo wamewashiwa vifaa hivyo na kuweza kusikia sauti kwa mara ya kwanza tangu wazaliwe.
Mbali na zoezi hilo, pia mtoto Uebert Kigala amerekebishiwa sauti kifaa alichopandikiziwa kwa ajili ya kumsaidia kusikia ikiwa ni mwendelezo wa wataalam kufuatilia maendeleo yake ili kuhakikisha kifaa kinafanya kazi kwa ufanisi.
Akizungumza na waandishi wa habari Daktari Bingwa wa Upasuaji Masikio, Pua na Koo Godlove Mfuko, amesema mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu Hospitali ya Mloganzila ilifanya upasuaji kwa watoto watatu ambapo leo wawili wamewashiwa vifaa vyao ili waweze kusikia sauti.
“Hawa watoto hawajawahi kusikia sauti tangu wazaliwe hivyo leo wataanza kusikia sauti mbalimbali katika mazingira yanayowazunguka baada ya kuunganisha vifaa hivi na kuviwasha’’ amefafanua Dkt. Mfuko.
Sambamba na hilo, Dkt. Mfuko ametoa wito kwa jamii kujenga utamaduni wa kupima afya zao kwa sababu asilimia 20 ya watu wenye tatizo la usikivu ndio wanaokuja hospitali huku asilimia 80 wakibaki nyumbani.
Tangu kuanzishwa kwa huduma hii Juni 2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jumla ya watoto 34 wamewekewa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlear Implants) hivyo kufanyika kwa huduma hizi nchini ni mwendelezo wa kuunga mkono jitihada za Mh. Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Joseph Pombe Magufuli za kuhakikisha wananchi wanafikiwa kwa urahisi.
Hadi sasa uwezo wa watalaam wazalendo kufanya upasuji umefikia asilimia 90 huku uwezo wa kuwasha vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implants) watoto waliopandikizwa vifaa hivyo ambao walizaliwa wakiwa hawasikii umeongezeka kufikia asilimia 100.
Gharama za upasuaji kwa mgonjwa au mtoto mmoja kuwekewa kifaa cha kusaidia kusikia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni Tshs. 36 milioni wakati akipelekwa nje ya nchi kwa matibabu hayo yanagharimu takribani Tshs. 80 hadi Tshs. 100 milioni kwa mtoto mmoja.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana