Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally
akitoa salamu za Chama wilayani Muleba kata ya Mayondwe katika shughuli ya dua iliyojumuisha maombi mbalimbali pamoja na kuiombea amani nchi yetu.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally akizungumza na baadhi ya wadau wa amani mara baada kutoa salamu za Chama wilayani Muleba kata ya Mayondwe katika shughuli ya dua iliyojumuisha maombi mbalimbali pamoja na kuiombea amani nchi yetu.
======== ======== ======== =======
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amewaeleza vijana umuhimu wa kuwa na maarifa kwani ukiwa na shahada pekee sio pesa, ila maarifa yako ndio hutengeneza pesa, hivyo vijana ni lazima wawe wabunifu, bila kuchapa kazi maisha yataendelea kubana.
Dkt. Bashiru amesema, yeye ni Katibu Mkuu wa CCM kwa sasa, lakini hakuna magulio asiyoyafahamu wilayani Bukoba, kwa kuwa alipokuwa anasoma na baada ya kuhitimu masomo yake, kazi kubwa aliyokuwa akiifanya bila uwoga ni uchuuzi kwenye magulio kazi ambazo vijana wengi wakiwa na shahada kichwani hawawezi kuzifanya.
Dkt. Bashiru ameyasema hayo, Desemba 29, 2019 alipokuwa akitoa salamu za Chama wilayani Muleba kata ya Mayondwe katika shughuli ya dua iliyojumuisha maombi mbalimbali pamoja na kuiombea amani nchi yetu.
“Vijana bila kuchapa kazi maisha yatabana, na vyuma vitabana kwelikweli, mimi ni Katibu Mkuu kwa sasa hakuna magulio nisiyoyafahamu hapa Bukoba na Muleba kwa kiasi, wakati nasoma na baada ya kuhitimu masomo kazi kubwa niliyoifanya kwa muda mrefu ni uchuuzi kwenye magulio kazi ambayo vijana wengi wakiwa na shahada kichwani hawapendi kuzifanya.’’ Bashiru ameeleza
Ameongeza kuwa, ukiwa na elimu ya shahada kichwani hiyo sio pesa, ila maarifa yako ndio yatatengeneza pesa akimtolea mfano Bw. Jafari Swalehe waliosoma naye darasa moja shule ya msingi Katerero na kuishia darasa la saba mkazi wa Bukoba vijijini ambaye kwa sasa ni mkulima mkubwa wa mbogamboga na matunda wilayani hapo.
Wakati huo huo, Dkt. Bashiru ameeleza wazi kuwa, CCM inajukumu la kutunga Sera wezeshi ili kundi kubwa la vijana waweze kupata mazingira mazuri ya fursa mbalimbali zikiwemo biashara, kilimo na viwanda, ambalo wameendelea kulifanya na katika Sera na Ilani ijayo suala hili litapewa uzito wa pekee ili kuwezesha kundi kubwa la vijana kupata na kumudu fursa za kimaendeleo.
Aidha, Dkt. Bashiru katika salamu hizo amehimiza upendo miongoni mwa wanafamilia na jamii kwa ujumla, ambapo ameeleza kuwa, maisha yetu ya upendo na undugu hutegemea maisha yetu ya kila siku, maisha ya upendo hutengenezwa katika ndoa, shule, siasa, biashara na maeneo mengine. Unayempenda huwezi kumfitini na utapenda afanikiwe, na vitabu vya dini zote vinahimiza upendo, hata CCM inahimiza upendo, kukemea chuki na fitina.
Awali kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, Shekhe Nuran Amri, akitoa neno la ukaribisho, amesisitiza kuwa, utofauti mkubwa wa binadamu na wanyama ni akili, binadamu tumepewa uwezo wa kutambua kibaya na kizuri, amani na fujo, chuki na upendo, hivyo hatuna budi kuitunza amani yetu, na kuwaombea viongozi wetu wakiongozwa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli ili wazidi na waendelee kuwa na upendo na uwajibikaji wa haki kama ilivyo sasa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na waumini wa dini zote viongozi mbalimbali wakiongozwa na Kaimu Shekhe wa Wilaya ya Muleba Bw. Hashim Haruna na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo Ndg. Athuman Kahara.
Katibu Mkuu yupo Bukoba Mkoani Kagera kwa mapumziko ya siku kumi ambapo anatarajiwa kumaliza mapumziko hayo mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020.
Post a Comment