WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Ayoub Mohammed Mahmoud awachukulie hatua watumishi wote watakaobainika kufanya ubadhilifu wa fedha za mapato ya Serikali.
Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma katika ngazi mbalimbali wajiimarishe katika ukusanyaji wa mapato na wahakikishe fedha zote zinazopatikana zinaingizwa kwenye mfuko wa Serikali.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Januari 17, 2020) wakati akizungumza na watumishi, viongozi wa mkoa wa Kusini Unguja katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, eneo la Tunguu.
Waziri Mkuu ambaye yuko Unguja kwa ziara ya kikazi, amesema ni muhimu kwa watumishi kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.
“Mkuu wa Mkoa usiogope chukua hatua kwa mtumishi yeyote atakayebainika kula fedha za mapato ambazo zinatolewa na wananchi kwa njia ya kodi. Mtumishi wa aina hiyo hafai kuwa mtumishi wa umma.”
Waziri Mkuu amemtaka kila mtumishi wa umma awajibike katika kufanya kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu na haitosita kuwachukulia hatua.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanasimamia vizuri uwajibikaji na utowaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.
Amesema huduma za jamii kama za afya, maji lazima ziimarishwe nchini na viongozi wa halmashauri wahakikishe zinapatikana ipasavyo. “Huduma zikiwa zinatolewa vizuri wananchi hawatolalamika.”
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Ayoub alisema halmashauri za wilaya zimeendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kutoa huduma kwa jamiii kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Kusini ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka sh. milioni 241 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi sh. milioni 524.51 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 118.
Alisema, kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kati ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka sh. milioni 304.27 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi kufikia sh. milioni 632.89 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 108 ya ukusanyaji wa mapato.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Post a Comment