Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kulia) amewataka wananchi wa Mji wa Mbalizi mkoani Mbeya kujikita katika kushiriki shughuli za maendeleo ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo mjini Mbalizi mkoani Mbeya alipokuwa akishiriki katika ujenzi wa vyumba tisa vya Madarasa ya Shule ya Sekondari Utengule Usongwe kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali inaendelea kuamsha ari ya wananchi katika kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuwaunga mkono pale wanapoanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.
"Wizara hii inahusika na masuala yote ya maendeleo ya kazi yetu kubwa ni kuamsha ari ya wananchi katika kujitolea na kushiriki katika shughuli za maendeleo" alisema Dkt. Ndugulile
Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali ya Awamu ya tano inataka kuona wananchi wanafanya kazi wanajishugulisha na shughuli za mendeleo kwa kuchangia katika miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Bw. Benedict Mahenge ameishukuru Serikali wananchi na wadau walijitolea katika kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo kwani itasaidia kupunguza adha ya wanafunzi kukaa wengi katika darasa moja.
Aidha Afisa Elimu Kata ya Utengule Usingwe George Mtawa amesema ujenzi wa vyumba vya madarasa tisa umekuja kutokana na kuwa na idadi kubwa ya shule za msingi na ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba hivyo wananchi waliamua kuanza ujenzi huo ili kuondokana na changamoto ya watoto kukosa madarasa ya kusomea.
Naye Diwani wa Kata ya Utengule Usongwe Elia Mkono amesema kuwa wananchi wa Kata hiyo wameamua kujenga vyumba vya madarasa hayo ili kuhakikisha watoto 981 wanapata madarasa ya kuanza kidato cha kwanza katika Shule hiyo.
Post a Comment