Ghasia za usiku wa tarehe 18 ya mwezi huu kati ya waandamanaji na maafisa usalama huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon, kwa akali zimepelekea watu 200 kujeruhiwa.
Duru mpya ya maandamano nchini humo ilianza Jumatatu iliyopita ya tarehe 13 Januari, hata hivyo siku ya Jumanne waandamanaji walitoa mwito wa kufanyika maandamano makubwa zaidi dhidi ya serikali na kuyataja kuwa ya 'Wiki ya Hasira.' Maandamano ya siku chache zilizopita pia yalikumbwa na mapigano kati ya maafisa usalama na waandamanaji kiasi kwamba makumi ya watu walijeruhiwa na makumi ya wengine kutiwa nguvuni. Swali muhimu ni hili kwamba, je, ni nini sababu ya kuibuka duru mpya ya maandamano ya wananchi dhidi ya serikali? Inaonekana kwamba kuna sababu mbili zilizochochea hali hiyo zikijumuisha siasa za kiuchumi za serikali ya Saad Hariri na kufeli kwa juhudi za Hassan Diab, Waziri Mkuu mpya aliyepewa jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri nchini humo. Serikali ya Saad Hariri hivi karibuni na kwa lengo la kudhibiti mgogoro wa kifedha, ilimuruhusu mtu kuweza kutoa dola 1000 pekee kwenye akaunti yake ya benki, siasa ambayo inatajwa kuwa sababu ya kuibuka kwa duru mpya ya maandamano nchini Lebanon. Ni kwa ajili hiyo ndio maana katika duru hii ya maandamano, waandamanaji wakaelekeza malalamiko na hasira zao kwa benki kuu ya Lebanon.
Maandamano nchini lebanon yaliyoanza tarehe 17 Oktoba mwaka jana na kupelekea kujiuzulu Saad Hariri, chanzo chake pia kilikuwa ni matatizo ya kiuchumi ambapo wananchi walimiminika mitaani kulalamikia hatua ya kuwekwa tozo ya kodi kwa ajili ya matumizi ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp. Suala hilo linaashiria kwamba suala la uchumi na ughali wa maisha, ndio chanzo kikuu cha maandamano nchini Lebanon. Hivi sasa Walebanon wanaamini kwamba miezi mitatu tangu kulipoanza maandamano nchini humo si tu kwamba hakujapatikana mabadiliko yoyote katika siasa za uchumi za serikali, bali mibano mipya ya kifedha imesababishwa matatizo mengine ya kiuchumi. Pamoja na hayo Jumanne ya wiki jana Rais Michel Aoun wa lebanon alitoa radiamali kufuatia kuanza duru mpya ya maandamano ambapo kwa mara nyingine amesema kuwa, Lebanon sasa inalipa gharama za siasa mbovu za kifedha za miaka 30 iliyopita. Kutoundwa baraza jipya la mawaziri ni sababu nyingine ya kuibuka kwa duru mpya ya maandamano nchini Lebanon. Hassan Diab aliruhusiwa kuunda baraza jipya la mawaziri tarehe 19 Disemba mwaka jana, lakini licha ya kupita mwezi mmoja sasa bado hajafanikiwa kutekeleza jukumu hilo. Alkhamisi iliyopita kuliripotiwa habari kwamba baraza jipya litatangazwa ndani ya mwezi huu, lakini hakuna kiongozi rasmi wa serikali aliyethibitisha habari hiyo.
Hivi sasa waandamanaji nchini Lebanon wanataka kuhitimishwa makundi ya kisiasa yanayoshadidisha tofauti nchini na badala yake kuharakishwe mwenendo wa kuundwa serikali mpya. Suala muhimu ni kwamba, kwa kuzingatia kuwa maandamano ya nchi hiyo huandamana na ghasia ambapo hata katika maandamano ya usiku wa tarehe 18 ya mwezi huu mjini Beirut yalikuwa ya ghasia kubwa ikilinganishwa na machafuko ya miezi mitatu iliyopita, hivyo maandamano yajayo yanatazamiwa kuwa na matokeo mabaya zaidi kwa nchi hiyo ya Kiarabu. Jambo muhimu ni kwamba ghasia hizo zinaweza kusababisha kuchelewesha zaidi uundwaji wa baraza jipya la mawaziri. Katika mazigira hayo, ghasia hizo zinaweza kuibua mpasuko zaidi kati ya wananchi nchini humo. Nukta ya kumalizia ni kwamba madola ya kigeni hadi sasa yamenyamazia kimya ghasia hizo na hivyo kuonyesha kwamba yanaridhishwa na hali hiyo kwa kuwa yanataraji kwamba machafuko hayo yatapelekea kufeli juhudi za Hassan Diab za kujaribu kuunda serikali mpya ya Lebanon, suala ambalo linafuatiliwa kwa karibu sana na muhimili wa Saudia, Israel na Marekani.
Post a Comment