Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kampeni ya kutangaza mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano inayojulikana kama 'Tunaboresha Sekta ya Afya' mapema leo Jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi anayesimamia Idara ya Huduma ya usimamizi wa vinasaba, David Eliasi akizungumza katika tukio hilo.
Viongozi mbalimbali wa Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Maabara ya Serikali wakiwa katika mkutano huo
NA ANDREW CHALE
MAMLAKA ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) ipo katika mkakati wa kuanzisha Kanzi Data ya taifa ya Vinasaba vya Binadamu (DNA) ambayo itakuwa ikitambua asili ya kila Mtanzania na kuweza kusaidia chunguzi mbalimbali ikiwemo majanga na kupata majibu kwa kina.
Hayo yameelezwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko wakati wa ziara ya kampeni ya kutangaza mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano inayojulikana kama ‘Tunaboresha Sekta ya Afya’ ambapo amesema kuwa;
Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha wanafikia malengo ya kusaidia jamii katika upande huo wa vinasaba.
"Kwa sasa tupo katika mpango wa kuanzisha Kanzi Data ya Taifa ya Vinasaba ambapo eneo hilo kwa sasa tutaliwekea kipaumbele katika bajeti ya fedha ya mwaka huu na tayari tumeshaanza kutengeneza mpango kazi wazo dhana ya utengenezaji wake na itajumlisha wadau mbalimbali na Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wengine". Alisema Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Mafumiko.
Dkt. Mafumiko amebainisha kuwa, kutokana na mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano kwa kuboresha rasilimali watu, miundombinu ya utendeajji kazi na vifaa vya kisasa ndio maana wamepewa jukumu hilo la kuanzishwa kwa Kanzi data hiyo sambamba na kujumuisha wadau mbalimbali.
Nae Mkurugenzi anayesimamia Idara ya Huduma ya usimamizi wa vinasaba, David Eliasi akizungumzia suala hilo la Kanzi data, amesema kuwa, Mkemia wa Serikali ndio atakuwa msimamizi na inajengwa na watanznia wenyewe huku akiwataka watanzania wajivunie juu ya hilo.
"Serikali ya awamu ya Tano imeweza kuongeza chachu na sasa tunajenga kanzi data ya Kitaifa ya Vinasaba na inajengwa na Watanzania wenyewe.
Ni kitu cha kujivunia na timu ya Kitaifa inasimamia huu ujenzi wakiwemo Wizara ya Afya ambayo ni mlezi wetu, pia wapo EGav- Serikali mtandao, NIDA, RITA, NEC na taasisi nyingi tu na wote hao wamekaa pamoja na wamekuja na dhana ya uanzishwaji wa Kanzi data hii ya Kitaifa" alisema David Eliasi.
Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa kanzi data hiyo, itarahisisha upatikanaji wa haraka wa majibu ya vinasaba kwani tayari sampuli zitakuwa zinapatikana kwenye data.
"Tutachukua muda mfupi na wa haraka zaidi. Mfano lile janga la Morogoro la moto, ndugu wa marehemu wangepatikana kupitia kanzi data hii na tungelipata majibu kwa haraka na kwa wingi zaidi" alisema Davidi Eliasi.
Aidha, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imenunua mitambo tisa kwa gharama ya shilingi bilioni 9.5 kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kemikali, sumu, madawa ya kulevya na viambata.
Ambapo pia imeweza kusajili wadau 2426 mwaka 2019 kutoka wadau 4340 mwaka 2015/2016.
Mpaka sasa Mamlaka hiyo ya Mkemia Mkuu imeendelea kuboresha huduma zake ikiwemo katika Kanda ya Ziwa, Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine ya Kanda.
Post a Comment