Kuzinduliwa mpango wa Kizayuni na Kimarekani wa "Muamala wa Karne" kumelaaniwa na nchi na shakhsia wengi wa kisiasa katika pembe mbali mbali za dunia.
Rais Donald Trump wa Marekani jana alichukua hatua ya upande mmoja bila kujali kugonga mwamba juhudi zake za miezi kadhaa za kutafuta uungaji mkono wa kieneo na kimataifa pamoja na ridhaa ya mirengo ya Palestina, kwa kuamua kuzindua mpango wa Kizayuni alioupa jina la "Muamala wa Karne".
Sami Abu Zuhri, mjumbe mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, matamshi aliyotoa rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mpango wa amani uitwao 'Muamala wa Karne' ni upuuzi usio na thamani yoyote na akaongeza kuwa Baitul Muqaddas itabaki kuwa ardhi ya Wapalestina.
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetoa taarifa na kusisitiza kwamba, hakuna njama, muamala na uhaini wa aina yoyote utakaoweza kuwanyang'anya Wapalestina haki zao kuhusiana na ardhi zao.
Hizbullah imeeleza katika taarifa yake kuwa, kama si njama na uhaini wa siri na wa dhahiri uliofanywa na baadhi ya tawala wa Kiarabu, 'Muamala wa Karne' usingekuwepo na ikaongeza kuwa, mpango hao muovu utakuwa na matokeo hatari kwa mustakabali wa eneo.
Sayyid Ammar al-Hakim, kiongozi wa harakati ya Hekima ya Kitaifa ya Iraq amesema, mpango wa 'Muamala wa Karne' ni njama hatari dhidi ya uthabiti na amani ya dunia.
Al-Hakim amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Taasisi za Kimataifa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuchukua msimamo wa kihistoria wa kulaani mpango huo wa Muamala wa Karne.
Kiongozi wa harakati ya Sadr nchini Iraq, Muqtada Sadr amesisitiza kuwa Quds tukufu inazihusu dini zote za tauhidi; na Palestina ni ardhi ya watu waliohuru.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema, ni muhali kupatikana amani bila Wapalestina kupatiwa haki zao ikiwemo kuunda nchi yao huru na yenye mamlaka ya kujitawala.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Assafadi yeye amesema, nchi yake inataka amani ya kweli na ya kiadilifu kulingana na maazimio ya kimataifa, itakayojumuisha kukomeshwa ukaliaji ardhi kwa mabavu na kulindwa haki za watu wa Palestina.
Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, Muhammad Abdussalam amesisitiza kuwa, mpango huo wa Muamala wa Karne ni uvamizi na uchokozi wa dhahiri dhidi ya Palestina na umma wa Kiislamu unaolenga kupanua ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Israel na uliofadhiliwa kifedha na Saudi Arabia na Imarati kwa madhumuni ya kuifuta kadhia ya Palestina.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeeleza katika taarifa rasmi iliyotoa kwamba, mpango wa 'Muamala wa Karne' umezaliwa ukiwa tayari ni mfu na kusisitiza kwamba, Ankara haitaruhusu utawala wa Kizayuni upate kisingizio cha kuhalalisha ukaliaji wake ardhi kwa mabavu na maudhi unayowafanyia Wapalestina na itaendeleza juhudi za kupatikana nchi huru ya Palestina.
Mpango wa kihaini wa 'Muamala wa Karne' unaokidhi matakwa ya utawala haramu wa Israel na kufuta haki za wananchi madhulumu wa Palestina umeandaliwa na serikali ya Marekani kwa ushirikiano na maafikiano na baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, Bahrain na Imarati.
Kwa mujibu wa mpango huo, mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) utahodhiwa na utawala wa Kizayuni, wakimbizi wa Kipalestina walioko nje ya Palestina hawatokuwa na haki tena ya kurudi kwenye ardhi zao za jadi na Palestina itakuwa sehemu iliyosalia ya maeneo ya Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan tu na Ukanda wa Gaza.../
Post a Comment