Wizara ya Mambo ya Nje ya Venezuela imeitahadharisha Marekani kutokana na tabia zake za kuendeleza mzingiro dhidi ya eneo la Amerika ya Latini na ukanda wa Karibiani.
Jorge Ariza ameyasema hayo baada ya kukutana na Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China mjini Beijing na kubainisha kwamba, lengo la Washington katika kutekeleza mzingiro wake endelevu katika eneo la Amerika ya Latini na Ukanda wa Karibiani, ni kutwaa utajiri wa maliasili za eneo hilo sambamba na kuziingiza madarakani serikali zinazodhamini maslahi ya Marekani. Ariza ameongeza kwamba daima Amerika ya Latini imekuwa ikikabiliana na mapinduzi ya kijeshi, hatua za kuibua mizozo, ugaidi, vita visivyo na mlingano na mzingiro wa kiuchumi, kibiashara na kifedha kutoka kwa Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesisitiza kwamba: "Sisi tunakaribisha muungano na nchi kama vile China katika nyuga tofauti.
Tunaamini kwamba kwa uungaji mkono wa China, serikali ya Caracas itaweza kuimarisha sekta zake za uzalishaji na pia kufufua uchumi wake." Tangu Venezuela ilipowekewa vikwazo vipya na Marekani katika kipindi cha Rais Donald Trump, imekuwa ikifanya juhudi kubwa kupitia stratijia mpya ya kupanua ushirikiano na waitifaki wake ikiwemo China na Russia ili iweze kufelisha siasa za kimabavu za Washington. Tangu mwanzoni mwa mwaka jana ambapo Marekani na washirika wake waliiwekea vikwazo serikali ya Caracas na kuwaunga mkono wapinzani, nchi hiyo ya Magharibi pia imekuwa ikifanya njama za kuiondoa madarakani serikali ya Rais Nicolás Maduro wa Venezuela ambayo inapinga siasa za kibeberu za Marekani.
Post a Comment