Na Maiko Luoga Mbeya
Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson Januari 21, 2020 alifanya ziara ya Kikazi katika kituo kikuu cha Mabasi mkoani Mbeya kwa lengo kutimiza ahadi yake ya kuwapatia Sare maalumu za kuwatambulisha maafisa usafirishaji katika jiji la Mbeya.
Maafisa hao maarufu kama Wapigadebe, wamepewa Sare hizo ili kuwaepusha na kero za kukamatwa mara kwa mara na Askari wa Jiji la Mbeya wakiwa hawana utambulisho maalumu wa kazi wanazozifanya wawapo kwenye Majukumu yao.
Aidha Dkt. Tulia amejionea na kuelezwa Changamoto mbalimbali zilizopo katika kituo hicho kikuu cha Mabasi ikiwemo ukosefu wa maji, ubovu wa miundombinu ya vyoo, uhaba wa taa kwaajili ya mwanga Majira ya usiku pamoja na Runinga maalumu ya kuwawezesha kufuatilia Taarifa na Matukio mbalimbali ya Kitaifa.
Changamoto nyingine ni pamoja na Ukosefu wa Vitendea kazi vya kubebea Mizigo ndani ya Stendi ikiwemo Toroli huku wakimuomba Naibu Spika Dkt, Tulia Ackson kuwawezesha upatikanaji wa mikopo kupitia Taasisi yake ya Tulia Trust.
Baada ya kuzungumza nao Dkt. Tulia ameahidi kushirikiana na Maafisa hao katika kutatua changamoto hizo huku akiwakabidhi Toroli moja la kubebea mizigo, kununua Taa za kufunga maeneo yanayozunguka kituo hicho cha Mabasi na kueleza kuwa atafanya jitihada za kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa haraka Kituoni hapo.
“Ndugu zangu niseme tu kwamba nimezisikiliza changamoto zenu na sisi kama Tulia Trust tunaahidi kushirikiana na Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt, John Pombe Magufuli kuhakikisha tunawakomboa vijana katika janga la umasikini, na hata hili suala la mikopo vijana wa Tulia Trust watakuja hapa na kuwapa huduma”-Alisema Dkt, Tulia Ackson Naibu Spika.
|
Post a Comment