Featured

    Featured Posts

NAIBU WAZIRI MABULA AZITAKA HALMASHAURI KUPANGA MIJI KUEPUKA MIGOGORO

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi wa Halmashauri za mkoa wa Kigoma jana wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma Vedastus Makota na kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Kigoma Samson Anga.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua moja ya Jalada la Ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya Kigoma jana wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Dkt Sebastian Siwale na kulia ni Karani wa Masijala ya Ardhi Haiba Mramba.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga (Kushoto) nje ya Ofisi ya Mkuu wa mkoa jana wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioneshwa baadhi ya nyaraka na Mchunguzi Mwandamizi wa TAKUKURU Kigoma Leonida Mshema kuhusiana na madai ya kuwepo udanganyifu kwenye hati ya ardhi ya umiliki wa eneo lilikuwa likimilikiwa na Shirika la National Milling eneo la Kibirizi Kigoma. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kigoma Samson Anga na kushoto ni Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Magharibi Thomas Antapa.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozwa na Mkuu wa wilaya ya Kigoma Samson Anga (wa pili kulia) kuelekea kuangalia  sehemu ya eneo lililokuwa likimilikiwa na Shirika la National Milling lililopo Kibirizi Kigoma, alipolitembelea jana baada ya kuelezwa kuwepo madai ya udanganyifu kwenye hati ya umiliki wa ardhi katika eneo hilo.


Na Munir Shemweta, WANMM KIGOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka Halmashauri nchini kuhakikisha zinapanga, kupima na kumilikisha ardhi ili kuepuka migogoro ya ardhi pamoja na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.
Dkt Mabula alitoa agizo hilo jana mkoani Kigoma wakati akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi wa halmashauri nane za mkoa huo akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Halmashauri hizo ni Buhigwe, Kasulu DC, Kasulu TC, Kakonko, Kibondo, Kigoma DC, Kigoma MC, na Uvinza DC.
Alisema, wakurugenzi wa halmashauri wanapaswa kutambua kuwa wana jukumu la kusimsmia halmashauri zao ili ziwe na miji yenye mpangilio mzuri ambapo alibainisha kuwa kama maeneo ya miji hiyo yataachwa bila kupangwa, kupimwa na kumilikishwa basi yatakuwa hovyo na maeneo mengi kuingia kwenye zoezi la urasimishaji.
‘’ Halmashauri zote nchini jukumu la kupanga miji ni la kwenu Wizara itasimamia nidhamu na ajira na mkizubaa katika hili miji itaendelea kuwa mibaya na serikali haitaki kuona ujenzi holela ukiendelea’’ alisema Naibu Waziri Mabula.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, urasimishaji unaofanyika sasa katika maeneo mbalimbali umesababishwa na kasi ndogo ya upangaji miji unaofanywa na halmashauri na kinachofanyika katika zoezi hilo ni huruma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi na kubainisha kuwa mwisho wa zoezi la urasimishaji ni mwaka 2023.
Alisema, hata idadi ndogo ya hati zilizotolewa katika halmashauri za mkoa wa Kigoma ni ishara ya kasi ndogo ya upangaji na upimaji katika mkoa wa Kigoma ambapo Naibu Waziri Mabula alishangazwa na halmashauri za Kigoma DC na Kasulu DC kwa kushindwa kutoa hata hati moja katika kipindi cha nusu mwaka huku halmashauri ya Buhigwe ikitoa hati sita tu na hivyo kuutaka mkoa kuhakikisha unazisimamia halmashauri hizo ili ziweze kupanga, kupima na kumilikisha maeneo mengi zaidi.
Kuhusu suala la mapato ya kodi yataokanayo na ardhi, Naibu Waziri Mabula ameoneshwa kutofurahishwa na kasi ya ukusanyaji mapato katika mkoa wa Kigoma ambapo kwa kipindi cha nusu mwaka 2019/2020 halmashauri za mkoa huo zimekusanya shilingi milioni 312,233,500.9 sawa na asilimia 13 tu huku Kigoma DC na Kasulu DC zikiwa zimekusanya mapato ya ardhi chini ya asilimia 1.2 na halmashauri pekee iliyofanya vizuri ni Kakonko iliyokusanya milioni 17,281,142.59 sawa na aslimia 28.
‘’Kama taasisi nyingine za serikali kama TRA zingekuwa hazikusanyi kodi kama ulivyo mkoa wa Kigoma katika suala la ardhi ambapo mna asilimia 13 tu basi miradi mikubwa inayofanywa kwa kutumia kodi za ndani ingekwama’’ alisema Dkt Mabula.
Awali Afisa Ardhi wa mkoa wa Kigoma Jairo Pilla katika taarifa yake ya nusu mwaka 2019/2020 ya utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Kigoma alisema, kiwango kidogo cha kodi ya ardhi kilichokusanywa kwenye mkoa wake kimesababishwa na sehemu kubwa ya ardhi kwenye mkoa huo kutopimwa na kumilikishwa.
Aidha, alisema suala lingine lilichongia mapato kidogo ya ardhi ni idara ya ardhi kutopewa kipaumbele na halmashauri za mkoa huo ambapo hakuna bajeti inayotengwa kwa ajili ya kupanga na kupima maeneo na kitu pekee kinachofanyika ni zoezi la urasimishaji na kusisitiza michoro mingi inayowasilishwa ni ya urasimishaji tu.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana