Featured

    Featured Posts

OFISA BIASHARA WILAYA YA IKUNGI ASIMAMISHWA KAZI KWA TUHUMA ZA KUTAFUNA FEDHA ZA MACHINGA

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika kikao kazi, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo leo. Kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa.



Na Happiness Shayo, Ikungi-Singida
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, amemsimamisha kazi Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Paulo Makaka kupisha uchunguzi wa tuhuma za kutumia fedha za wamachinga kwa maslahi binafsi.

Dk. Mwanjelwa amechukua hatua hiyo leo wakati wa kikao kazi kati yake na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

“Ninaagiza Afisa Biashara huyu asimamishwe kazi wakati taratibu nyingine za kiutumishi zinaendelea na ninatoa mwezi mmoja kwa Kamanda wa TAKUKURU kufanya uchunguzi na kuwasilisha majibu” Dk. Mwanjelwa amesisitiza.

Amefafanua kuwa Afisa Biashara huyo amekusanya fedha za vitambulisho zaidi ya 500 vya wamachinga pamoja na ushuru wao bila kuziwasilisha sehemu inayohusika. 

Pia, Afisa Biashara huyo amekuwa akitumia muda wa kazi vibaya kwa kuchelewa kuripoti kazini ambapo ni kinyume na taratibu za kiutumishi.

Dk. Mwanjelwa amesikitishwa na watendaji wa halmashauri hiyo wanaolalamikia ukosefu wa mapato wakati Afisa Biashara huyo amekuwa akitumia makusanyo ya serikali kwa matumizi binafsi.

Aidha, Dk. Mwanjelwa amewaasa  watumishi wengine kuacha kukiuka misingi ya kanuni na taratibu za kiutendaji kwa kuwa serikali haitawaacha salama wote watakaogungulika kukiuka misingi hiyo. 

Katika hatua nyingine, Dk. Mwanjelwa ametoa onyo kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wanaoishi nje ya kituo cha kazi na kuwataka kuhamia haraka iwezekanavyo katika eneo lao la kazi ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Ni marufuku kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kuishi nje ya kituo cha kazi kwa kuwa hili linapunguza ufanisi wa kazi  na huduma kwa wananchi hazitolewi ipasavyo kutokana na kuishi mbali” Dkt. Mwanjelwa amesema.

Mhe.Dkt. Mwanjelwa amehitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani Singida ambapo alitembelea Manispaa ya Singida na Halmashauri za Wilaya ya  Singida, Mkalama, Iramba na Ikungi. Lengo la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF pamoja na kuzungumza na watumishi, kusikiliza kero zao na kuzitatua.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © 2025 Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana