Kiongozi wa zamni wa Kanisa Katoliki Duniani amemtaka rasmi Papa wa sasa wa kanisa hilo kutupilia mbali mpango wa kuwaruhusu watu waliooa kutawazwa kuwa makasisi katika kanisa hilo.
Benedict XVI jana alimtaka rasmi Papa Francis kusitisha mpango wa Kanisa Katoliki wa kuruhusu wachungaji wenye wake kuwa makasisi kutokana na kile kinachosemekana kuwa ni upungufu wa viongozi wa kidini katika eneo la Amazon.
Papa Benedict, ambaye alistaafu mwaka 2013, amesema hawezi kunyamazia suala hilo.
Katika kitabu alichokiandika kwa kushirikiana na Kadinali Robert Sarah, Papa mstaafu Benedict amesema kutofunga ndoa kwa makasisi ni utamaduni wa kale ambao umekuwepo kwa karne nyingi tu ndani ya kanisa hilo, na kuna umuhimu mkubwa kwa sababu kunawaruhusu makasisi kuzingatia zaidi majukumu yao.
Mjadala huo ulianza baada ya Baraza la Kanisa katika eneo la Amazon huko America ya Latini kupendekeza kwa Vatican kuwa, wanaume wenye wake wa rika la kati na wazee wakubaliwe kuwa makasisi, suala ambalo limezusha malumbano baina ya viongozi wa Vatican kutokana na sharti la useja kwa mtu yeyote anayetawazwa kuwa kasisi katika kanisa hilo.
Papa Benedict mwenye umri wa miaka 92 amesema "Halionekani kuwa jambo linalowezekano kutimiza majukumu ya ukasisi na ndoa kwa wakati mmoja".
Upinzani dhidi ya kuwepo makasisi wenye wake katika Kanisa Katoliki unaandamana na mashinikizo makubwa ya walimwengu kwa viongozi wa kanisa hilo kutokana na kashfa za ngono na udhalilishaji wa watoto wadogo unaofanywa na makasisi katika maeneo mbalimbali duniani.
Post a Comment