Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd amesema serikali haitosita kuimarisha utoaji wa huduma za maji safi na salama kwa wananchi wake mpaka ihakikise kwamba lengo la usambazaji maji kwa jamii nchini linatekelezwa kama walivyodhamiriwa na waasisi wa Mapinduzi ya mwaka 1964.
Akizungumza kwa niaba Makamu wa Pili, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed huko Uroa Wilaya Kati Unguja katika hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa Maji Safi na Salama wa Bambi – Uroa ikiwa ni shamra shamra za kutimiza miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema kutokana na juhudi anazochukuwa Rais Dk. Shein za kuwaleta maendeleo wananchi wake serikali imelipa umuhimu tatizo la maji katika kijiji cha Uroa kwa kufanya jitihada kubwa za kukiendeleza kisima kilichochimbwa kupitia mradi wa visima uliofadhiliwa na Mtawala wa Ras-Al-Khaimah ili kuondoa kero ya maji kijijini humo
Amesema serikali inachukua juhudi mbali mbali katika kuendeleza na kuimarisha huduma bora za kijamii mijini na vijijini ikiwa ni utekelezaji wa miradi ya maendeeleo nchini.
Balozi Seif ameeleza kuwa upatikanaji wa huduma ya maji safi vijijini kutasaidia kuondosha changamoto zinazokumba wanawake na watoto wa kike kupata nafasi ya kujishughulisha na masomo yao, kuimarisha shughuli zao za maendeleo pamoja na kuijenga jamii katika afya bora.
Aidha amewataka wananchi wa kijiji hicho kuilinda na kuitunza miradi hiyo ili iwe endelevu na yenye kudumu na ili kuweza kufaidika vyema na matunda ya Mapinduzi kwa manufaa ya jamii na Taifa
Nae waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Mhe. Salama Aboud Talib amesema serikali inatumia gharama nyingi katika kuwaletea maendeleo wananchi hivyo Mamlaka ya Maji ZAWA inatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuhakikisha kuwa wananchi wake wanapata maji safi na salama mjini na vijijini.
Aidha wamewataka wananchi hao kuchangia huduma hiyo na kutumia kwa uangalifu pamoja na kuilinda miundombinu ya maji ili kuepuka uharibifu na kuweza kudumu kwa muda kwa maslahi ya jamii
Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizaya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Ali Halil Mirza mradi huo wa maji una uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita laki 9 kwa siku ambao umegharimu zaidi milioni 300 na umefadhiliwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Ras-Al-Khaimah.
Post a Comment