Mwenyekiti wa Kamati ya Upelelezi ya Kongresi ya Marekani amesema kuwa, Rais wa nchi hiyo Donald Trump ametoa ripoti za uongo ili kuhalalisha mauaji ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani.
Adam Schiff ambaye ni mwakilishi wa jimbo la California katika Kongresi ya Marekani ameiambia televisheni ya CBS News kwamba, Donald Trump na maafisa wengine wa serikali yake wanasema uongo ili kuhalalisha mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Upelelezi ya Kongresi ya Marekani ameashiria mahojiano ya Donald Trump na televisheni ya Fox News na kusema: Unapomuona Rais wa Marekani akisema maneno kama haya unaelewa kuwa anasema uongo.
Schiff ameongeza kuwa, Trump na watu wa karibu yake wanatia chumvi katika kadhia ya mauaji ya Jeneral Soleimani kwa shabaha ya kuhalalisha mauaji yake na suala hili yumkini likatuburuta katika vita na Iran, jambo ambalo ni hatari kubwa.
Akihojiwa na televisheni ya Fox News ya Marekani, Rais wa nchi hiyo, Donald Trump alijaribu kuhalalisha jinai yake hiyo kwa kusema: Iran ilikuwa ikipanga kushambulia balozi nne za Marekani ukiwemo wa mjini Baghdad.
Siku ya Jumapili iliyopita pia Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mark Esper alikanusha madai ya Trump ya kwamba Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa amepanga kushambulia balozi za Marekani na kusema kuwa, yeye kama waziri wa ulinzi wa Marekani, hana ushahidi wowote wa kuonesha kuwa, Iran ilikusudia kushambulia balozi nne za Marekani.
Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Abu Mahdi al Muhandes na wenzao wanane waliuawa kigaidi tarehe 3 mwezi huu wa Januari na jeshi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Jenerali Soleimani alikwenda Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (Sepah) lilijibu mauaji hayo ya kigaidi kwa kushambulia kambi kubwa zaidi ya jeshi la Marekani nchini Iraq ya Ainul Asad kwa makombora ya balestiki na kuisambaratisha.
Post a Comment