Umoja wa Ulaya sambamba na nchi tatu za Ulaya za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zinazojulikana kama Troika ya Ulaya, ni waungaji mkono wa mapatano ya kimataifa ya nyuklia maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Licha ya kuwa nchi hizo za Ulaya zimeshindwa kutekeleza ahadi zao za mapatano hayo baada ya Marekani kuijiondoa kwenye mapatano hayo mnamo Mei 2018, lakini bado zinasisitiza kulindwa kwake na hilo linatokana na umuhimu wa mapatano hayo. Kwa msingi huo nchi hizo wanachama wa kundi la 4+1 zimepinga vikali pandekezo na ombi lililotolewa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani akizitaka zijitoe kwenye mapatano hayo. Trump amedai kwamba anataka maafikiano mapya yafikiwe kati yake na wananchama wa kundi hilo ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kile alichodai kuwa yatachangia zaidi kudhamini amani na usalama wa dunia. Kufuatia kujitoa kwake kwa upande mmoja JCPOA Marekani imetangwa kikamilifu katika uwanja wa kimataifa kuhusiana na jambo hilo, na kufikia sasa imeshindwa kuzishawishi nchi nyingine zijitoe katika mapatano hayo.
Katika uwanja huo, Annegret Kramp-Karrenbauer, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, akiziwakilisha nchi za Ulaya ametupilia mbali ombi la Rais Trump la kuzitaka nchi hizo zijiondoe JCPOA na kusema kuwa mapatano hayo ni muhimu sana, ambapo yanazilazimu nchi zote kufanya juhudi za kuyalinda. Ujerumani, Ufaransa na Uingereza daima zimekuwa zikitangaza kwamba mapatano ya JCPOA ni muhimu na nyeti mno kiasi kwamba zinafanya kila zinaloweza ili kuyalinda. Pamoja na hali hiyo nchi hizo zenyewe zinafahamu vyema kwamba JCPOA haiko katika hali nzuri. Kutokana na ukweli huo, Kramp-Karrenbauer amesema: Iwapo fursa itaendelea kuwepo tunawajibika kufanya juhudi za kuilinda JCPOA na hili ni jambo ambalo linakubaliwa kwa pamoja na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.
Uingereza pia inakubaliana wazi na Ujerumani kuhusiana na suala hilo. Imepinga moja kwa moja takwa la kuitaka ijiondoe JCPOA na kusisitiza kwamba matapano hayo ya kimataifa yana umuhimu mkubwa kwa usalama wake wa kitaifa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilitangaza Alkhamisi kwa kusema: Licha ya kwamba tuna wasiwasi mkubwa na hatua ya karibuni ya Iran kupunguza zaidi vizuizi ilivyokuwa imewekewa katika mapatano ya nyuklia, lakini bado tunaitazama JCPOA kama mkataba muhimu wa usalama wetu wa pamoja na kwa ajili ya kuizuia Iran kuwa na nguvu ya atomiki. London inaamini kwamba malengo ya usalama ya JCPOA yanaweza kufikiwa kwa njia ya kidiplomasia na kwa kulindwa mapatano hayo.
Mtazamo huo wa Troika ya Ulaya pia umeungwa mkono na Umoja wa Ulaya. Akizungumzia jambo hilo Ursula von der Leyen, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya siku ya Jumatano alisisitiza umuhimu wa JCPOA na kudai kwamba Umoja wa Ulaya utafanya juhudi zake zote ili kuyalinda mapatano hayo ya kimataifa.
Baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika mapatano ya JCPOA Mwezi Mei 2018, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliahidi kuendelea kuyajeshimu kwa sharti kwamba nchi zilizosalia katika mapatano hayo nazo zitekeleze ahadi zao, lakini baada ya kupita karibu miaka miwli bila kuona uwajibikaji wowote wa wanachama wengine wa kundi la 4+1 na hasa nchi za Ulaya kuhusiana na kadhia hiyo, Iran iliamua kuweka pembeni subira yake ya kistratijia na kuchukua hatua ya kupunguza taratibu uwajibikaji wake katika mapatano hayo. Katika uwanja huo, tarehe 5 Januari, Iran ilitoa taarifa ikitangaza kuanza kutekeleza hatua ya tano na ya mwisho ya kupunguza uwajibikaji huo, ambapo sasa haitakuwa tena na kizuizi chochote kitakachoizuia kurutubisha kiwango chochote kile cha madini ya urani au kufanya utafiti na ustawi katika uwanja huo.
Kwa maelezo hayo, tokea sasa mpango wa nyuklia wa Iran utaendeshwa tu kwa msingi wa maslahi na mahitaji yake ya kitaifa. Ni wazi kuwa suala hilo litatekelezwa kwa ushirikiano kamili na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA kama ilivyokuwa huko nyuma. Pamoja na hayo Iran imetangaza wazi kuwa iko tayari kurejea katika uwajibikaji wake wa JCPOA iwapo itaondolewa vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa na Marekani na kuruhusiwa kunufaika na mapatano ya JCPOA. Akifafanua suala hilo. Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba Iran itaendelea kushirikiana na wakala wa IAEA katika uwanja huo.
Kwa msingi huo iwapo nchi za Ulaya zinataka kudhamini maslahi yao ya kiusalama, zinapaswa kutekeleza kivitendo ahadi zao ukiwemo mfumo wa mabadilishano ya kibiashara na kifedha na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaojulikana kama INSTEX, badala ya kutoa ahadi na maneno matupu yasiyotekelezwa.
Post a Comment