Wavutaji wa sigara au bidhaa za tumbaku wako katika hatari kubwa ya kupata masaibu na matatizo zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji kuliko wasiovuta bidhaa hizo.
Shirika la Afya Duniani WHO limetoa tahadhari hiyo na kusema miongoni mwa hatari hizo ni matatizo ya moyo na mapafu kushindwa kufanya kazi ipasavyo, maambukizi na kuchelewa kupona kwa mshono.
Taarifa hiyo imesema uchunguzi umebaini kuwa, watu ambao wanaacha kuvuta bidhaa za tumbaku wiki nne au zaidi kabla ya kufanyiwa upasuaji, hatari ya kupata matatizo mengine zaidi baada ya upasuaji hupungua na kuwa na matokeo mazuri miezi sita baadaye.
WHO imesema wagonjwa ambao huacha kabisa kuvuta bidhaa za tumbaku huwa hawakumbwi na matatizo wanapopatiwa dawa ya usingizi wakati wa upasuaji wakilinganishwa na wale ambao bado wanavuta bidhaa hizo.
Taarifa hii imetokana na utafiti wa pamoja wa WHO, Chuo kikuu cha Newcastle, Australia na Shirikisho la Anestesiologia Duniani (WFSA).
Dkt. Vinayak Prasad mkuu wa kitengo cha kupambana na matumizi ya tumbaku katika shirika la WHO amesema utafiti huo unaonyesha kwamba kila anayeishi bila kuvuta tumbaku kwa wiki moja, baada ya wiki nne huboresha afya yake kwa asilimia 19.
Post a Comment