Kundi moja la maveterani wa vita vya nje ya Marekani wamemtaka rais wa nchi hiyo Donald Trump aombe radhi kwa kudharau madhara waliyopata wanajeshi wa Marekani baada ya kambi yao ya Ain al Assad ya nchini Iraq kushambuliwa kwa makumi ya makombora ya Iran.
Wiki iliyopita Trump alikiri kwamba wanajeshi wa Marekani wamepata matatizo ya ubongo kutokana na mashambulizi hayo ya Iran na kudai kuwa matatizo hayo si lolote si chochote.
Hata hivyo dharau hiyo ya rais wa Marekani kwa madhara waliyopata wanajeshi wa nchi hiyo yamewakasirisha watu wengi nchini Marekani wakiwemo maveterani wa kivita ambao wamesema kuwa matatizo ya ubongo si jambo dogo hivyo Trump anapaswa kuomba radhi kwa kudharau maisha na usalama wa wanajeshi wa Marekani.
Tarehe 8 mwezi huu wa Januari 2020, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH lilishambulia kwa makombora kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani ya Ain al Assad huko magharibi mwa Iraq kujibu jinai ya wanajeshi magaidi wa Marekani ya kumuua kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds, cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq.
Hata hivyo katika juhudi za kupunguza mashinikizo ya ndani na ya kimataifa, Donald Trump alidai kuwa mashambulizi hayo hayakusababisha hasara zozote kwa wanajeshi wa Marekani. Pamoja na hayo, kadiri muda unavyopita ndivyo Ikulu ya Marekani, White House inavyozidi kukiri hasara kubwa zilizosababishwa na majibu hayo makali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Awali Washingtoni ilikiri kuwa wanajeshi wake 11 walipata matatizo ya ubongo. Siku chache zilizopita, Wizara ya Ulinzi wa Marekani imekiri tena kwamba wanajeshi 34 wa nchi hiyo wamepata matatizo ya ubongo baada ya mashambulizi hayo ya Iran.
Post a Comment