Featured

    Featured Posts

WATAKIWA KUBORESHA MAZINGIRA RAFIKI KWA WENYE ULEMAVU

   Chama cha Wabunge wenye ulemavu kimewapongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuendelea kusimamia vyema vivutio vya Mji Mkongwe na Kaole vilivyopo Bagamoyo huku kikiwataka wadau wa Utalii kutengeneza mazingira rafiki yatakayowawezesha watu wenye walemavu kufika kirahisi kutembelea hifadhi hizo.

Hayo yamezungumzwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa mara baada ya kutembelea katika vivutio hivyo huku akiwa ameongozana na wabunge wenzake wenye ulemavu ziara iliyokuwa imeratibiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Amesema kuwa ni vyema Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa utalii wanaosimamia hifadhi za Taifa na vitutio vya asilia akiwemo TFS, TAWA na TANAPA ni vyema kutengeneza miundombinu rafiki itakayoweza kuwasaidia watu wenye ulemavu nao kutembelea hifadhi hasa katika upande mambo ya kale.

"Napenda nitoe pongezi zangu kwa Kamishna Mhifadhi Mkuu wa TFS Prof. Dos Santos Silayo na timu yake kwa ujumla kwa kuweza kuwa na vijana mahili wanaojua kutoa elimu sahihi kwa wageni wanaotembelea katika hifadhi zote wanazosomamia ila niwaombe kuendelee kusimamia vyema huku mkitengeneza mazingira rafiki ya miundombinu ili kutuwezesha tufike kwa wingi kutembelea mambo ya kale," amesema Naibu Waziri Ikupa.

Ameongeza kuwa kwa sasa serikali haipo nyuma kuendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa hoteli, watoa huduma kwa jamii kuwapa kipaumbele walemavu ili nao waweze kujikwamua na wasonge mbele kimaendeleo kuliko kubaki wakiwa omba omba.

"Serikali ya Awamu ya Tano haipo nyuma katika kuwashika mkono walemavu ili waweze kusonga mbele kimaendeleo hivyo niwaombe wenzangu wenye ulemavu kuacha kulemaa na kubaki wakiwa omba omba bali wafanye kazi kwa bidii ili waweze kusonga mbele kujenga uchumi wa Taifa," Amesema Naibu Waziri Ikupa.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wenye Ulemavu Mhe. Riziki Lulida ambaye ni mmoja ya mabalozi wa Utalii ameishukuru TFS kwa kuweza kuwapa nafasi ya kutembelea vivutio hivyo huku ikiwaomba kuwasaidia vijana kuwawezesha kutumia misitu wanayoisimamia kuzalisha zao la asali ili waweze kujikwamua kiuchumi.

"Niwapongeze TFS kwa kutupa nafasi sisi wabunge wenye ulemavu kutembelea vivutio vya mambo ya kale ila endeleeni kuzalisha ajira kwa vijana kwa kuweza kupatia maeneo ili waweze kuzalisha zao la asali, unapowaweka wataendelea kutunza mazingira huku wakijikwamua kiuchumi," amesema Mhe. Lulida.

Amesema kwa sasa Wizara na Maliasili na Utalii ni vyema kuvisimamia vyema vivutio maana Utalii ndiyo zao pekee linaloleta pesa kwa nchi mbali na hapo zamani kilimo kilikuwa kinaongoza.

Kwa upande wake Meneja wa TFS Kanda ya Mashariki Bi. Caroline Malundo amewaomba Watanzania kujitokeza kutembelea vivutio vya misitu asili na mambo ya kale ili kuweza kujipatia elimu na historia ya kale ya mababu zetu.

Amesema kuwa katika jitihada za kukuza utalii na kukuza pato la Taifa, TFS kwasasa imeongezewa vivutio mbali na Misitu asilia pia imepewa dhamana ya kusimamia Magofu ya Kale yaliyopo mji Mkongwe na Kaole, Bagamoyo - Pwani, Michoro ya Miamba, Kolo- Kondoa, Magofu ya Tongoni - Tanga.

Aidha TFS imejipanga kusimamia na kuendeleza vyema vivutio vya mambo ya kale na kuweza kuvipa kipaumbele zaidi ili Watanzania wasiweze kupoteza historia ya mababu zetu.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana