Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imetangaza kuwa askari wasiopungua 20 wa linalojiita jeshi la taifa la Libya chini ya uongozi wa Jenerali Khalifa Haftar wameuawa katika mapigano ya kutaka kudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.
Taarifa iliyotolewa na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imesema kuwa, askari hao wameuawa katika mapigano yaliyojiri baina ya jeshi la Haftar na wapiganaji wa serikali hiyo kusini mwa Tripoli.
Katika mapigano makali ya Ijumaa iliyopita pia magari mawili ya deraya ya jeshi la Imarati yalipigwa na kuharibiwa.
Tangu mwezi Aprili mwaka 2019, vikosi vya Khalifa Haftar vinavyosaidiwa na kuungwa mkono na Saudi Arabia na Imarati na ambavyo vinashikilia eneo la mashariki ya Libya vilianzisha hujuma na mashambulio makali kwa madhumuni ya kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoti na kuiangusha Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj.
Hata hivyo tarehe 27 Novemba mwaka jana serikali ya Uturuki na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa zilisaini makubaliano ya kushirikiana kijeshi na katika masuala ya baharini, suala ambalo limetajwa na baadhi ya wachambuzi wa mambo kwamba yumkini likabadili mlingano wa kijeshi katika machafuko ya sasa huko Libya.
Post a Comment