Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Kwa Mwaka wa Fedha 2019/20 Halmashauri Kote nchini zilipanga kukusanya Shilingi Bilioni 765.48 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani ambapo Katika kipindi cha nusu mwaka (Julai hadi Desemba, 2019) Halmashauri zimekusanya Jumla ya Shilingi bilioni 356.81 ambayo ni asilimia 47 ya makisio ya mwaka.
Hayo yamesemwa leo Februari 9,2020 jijini Dodoma na Waziri wa TAMISEMI Mhe.Seleman Jafo wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha nusu mwaka [Julai –Disemba ,2019]kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
Waziri Jafo amesema Uchambuzi wa taarifa za mapato ya vyanzo vya ndani vya Halmashauri katika kipindi cha Julai - Desemba, 2019 umeonesha kuwepo kwa ongezeko la mapato yaliyokusanywa kwa kiasi cha Shilingi bilioni 56.7 ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho cha Julai - Desemba, 2018 sawa na ongezeko la asilimia 19.
Waziri Jafo amesema Uchambuzi unaonesha kuwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019 Halmashauri 63 kati ya Halmashauri 185 zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 50 na zaidi ya makisio kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 huku Halmashauri mia ishirini na mbili (122) zimekusanya mapato ya ndani chini ya asilimia 50 ya makisio ya mwaka.
Waziri Jafo ameendelea kufafanua kuwa Katika kipindi cha miezi sita (Julai – Desemba, 2019), Halmashauri za Wilaya za Tunduru na Kibondo zimekusanya mapato kwa asilimia 104 ya makisio ya mwaka 2019/2020 ambapo Halmashauri zote zilizokusanya zaidi ya asilimia 100 hadi Desemba, 2019 na zile ambazo zimejitathmini na kuona upo uwezekano wa kuzidi asilimia 100 ya bajeti za mapato ya ndani ifikapo Juni, 2020 zinaelekezwa kufanya mapitio ya Bajeti kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 ili ziweze kuongeza Bajeti za mapato na matumizi ya fedha hizo.
Aidha, Halmashauri za Wilaya za Mafia, Ukerewe na Gairo zimekusanya asilimia 18 tu ya makisio yake kwa kipindi cha miezi sita,
Katika kuzipima Halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Bilioni 29.75 na Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekusanya mapato kidogo kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Milioni 186.10.
Katika Taarifa ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri Kimkoa kwa Kuzingatia Asilimia ya Makusanyo,Mkoa wa Geita umefanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019 ambapo umekusanya wastani wa asilimia 63 ya makisio ya Halmashauri za Mkoa huo huku Mkoa wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mkoa wa Tanga ambao umekusanya wastani wa asilimia 36 ya makisio ya mwaka ya Halmashauri za Mkoa huo .
Kwa kigezo cha wingi wa mapato, Mkoa wa Dar es Salaam umefanya vizuri kwa kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 83.86. Mapato ya Mkoa yameongezeka kwa Shilingi Bilioni 6.45 ukilinganisha na makusanyo ya Julai – Desemba, 2018 na Mkoa wa mwisho katika wingi wa ukusanyaji wa mapato ni Mkoa wa Katavi ambao umekusanya Shilingi bilioni 4.68 katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019 lakini ukiwa ongezeko la Shilingi Bilioni 2.3 ukilinganisha na mapato yaliyokusanywa Julai – Desemba, 2018.
Katika kipindi hicho Kwa kigezo cha cha asilimia ndani ya halmashauri,Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongoza kundi la Halmashauri za Majiji kwa kukusanya mapato kwa asilimia 71 ya makisio yake ya mwaka huku Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya kwa asilimia 41 ya makisio yake ya mwaka
Waziri Jafo ameendelea kufafanua kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeongoza kundi la Halmashauri za Manispaa ambayo imekusanya asilimia 75 ya makisio yake huku Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma ikiwa ya mwisho ambapo imekusanya kwa asilimia 26 ya makisio yake kwa Mwaka wa Fedha 2019/20 .
Kwa upande wa Halmashauri za Miji, Halmashauri ya Mji wa Njombe imeongoza kwa kukusanya kwa asilimia 88 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2019/20 ambapo Halmashauri ya Mji wa Babati imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 30 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2019/20 .
Aidha, kwa kundi la Halmashauri za Wilaya, Halmashauri za Wilaya za Tunduru na Kibondo zimeongoza kwa kukusanya asilimia 104 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa Fedha 2019/20 wakati Halmashauri za Wilaya za Mafia, Ukerewe na Gairo zimekuwa za mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya asilimia 18 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa Fedha 2019/20.
Katika kipindi hicho Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongoza kundi la Halmashauri za Majiji kwa kukusanya Shilingi bilioni 29.75. Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi bilioni 6.03.
Kwa upande wa Halmashauri za Manispaa ya Ilala imeongoza kwa kukusanya Shilingi bilioni 29.13. Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 694.93.
Katika kipindi hiki, Waziri Jafo amesma Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa wingi wa Mapato katika Halmashauri za Miji ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 4.64. Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 459.44.
Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze imeongoza kwa kukusanya mapato mengi kwa Halmashauri za Wilaya ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 3.89. Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 186.08 .
Katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019 Halmashauri zimetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 228.48 ambayo ni asilimia 64 ya mapato halisi yaliyokusanywa kuanzia Julai hadi Desemba, 2019. Kati ya matumizi hayo, Shilingi Bilioni 137.56 zimetumika kwenye matumizi ya kawaida na Shilingi Bilioni 90.92 zimetumika kwenye matumizi ya maendeleo. Aidha, katika kipindi hicho kiasi cha Shilingi Bilioni 18.61 kimetumika kwenye miradi ya maendeleo ikiwa ni bakaa ya mapato ya ndani ya mwaka wa fedha 2018/19 ambayo ni asilimia 54 ya bakaa yote (Shilingi Bilioni 34.33), hivyo kufanya jumla ya matumizi ya miradi ya maendeleo kufikia Shilingi Bilioni 109.53.
Uchangiaji wa fedha za ndani katika shughuli za maendeleo umezigawa Halmashauri katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza ni Halmashauri zinazochangia asilimia 60 na kundi la pili ni Halmashauri zinazochangia asilimia 40 ya mapato ya ndani. Kama ilivyoelezwa hapo awali fedha zilizotumika katika miradi ya maendeleo kwa kipindi cha husika ni Shilingi Bilioni 90.92.
Uchambuzi wa taarifa hii unaonesha kuwa katika kundi la kwanza ambalo lina Halmashauri 16, Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa kuchangia asilimia 24 ya mapato halisi (own source proper) na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imekuwa ya mwisho kwa kuchangia asilimia 10 ya mapato halisi (own source proper).
Katika kundi la pili lenye Halmashauri 169, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo imeongoza kwa kuchangia asilimia 36 ya mapato halisi (Own source proper) na Halmashauri ya mwisho katika kundi hili ni Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ambayo imechangia asilimia 1 ya mapato halisi (own source proper). Aidha, Halmashauri nne za Wilaya za Buhigwe, Kakonko, Handeni na Missenyi hazijachangia kiasi chochote katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika Kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019 Halmashauri zilitoa Mikopo kiasi cha Shilingi Bilioni 14.12 kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ikiwa ni asilimia 12 ya Bajeti ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ambayo ni Shilingi Bilioni 62.36.
Halmashauri nane zilizoongoza katika kutoa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ni Halmashauri za Wilaya za Kibondo, Mlele, Mufindi, Mbarali na Njombe, Halmashauri za Manispaa za Ilala na Mpanda na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Halmashauri hizi zimechanga kati ya asilimia 7 hadi asimilia 10 ya mapato halisi (own source proper). Halmashauri za mwisho katika kutoa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ni Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri za Miji Kibaha na Mafinga ambazo zimechangia asilimia 1 ya mapato halisi.
Hata hivyo, zipo Halmashauri 37 ambazo hazijatoa kiasi chochote cha mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019. Orodha ya Halmashuri hizo imeambatishwa.
Waziri huyo wa TAMISEMI ameainisha baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kipindi cha Julai – Desemba, 2019 ni pamoja na ,Makisio yasiyoakisi hali halisi ya mapato yanayoweza kukusanywa ambapo baadhi ya Halmashauri zimeweka makisio makubwa au madogo bila kuzingatia hali halisi ya uwezo wa vyanzo vya mapato ya ndani hivyo kushindwa kukusanya kufikia malengo au kuonekana zimekusanya zaidi.,Baadhi ya Halmashauri hazisimamii kikamilifu matumizi ya mashine za kukusanyia mapato (POS);
Changamoto nyingine Waziri Jafo ambazo ameainisha ni ,Kushindwa kuweka mikakati madhubuti ya kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo vipya vinavyobuniwa na Halmashauri,Matumizi yasiyo sahihi ya mifumo ya kielektroniki ambayo inasababisha kutopatikana kwa taarifa sahihi na kwa wakati; naKuwepo kwa baadhi ya Halmashauri ambazo hazizingatii utaratibu wa kufanya usuluhishi wa mapato kwenye mifumo ya kielekitroniki kwa wakati.
Waziri Jafo amebainisha Mikakati ya Kutatua Changamoto ni pamoja na Mikoa inapaswa kuendelea kuzisimamia Halmashauri kutoa taarifa kupitia mifumo ya kielektroniki kwa kusisitiza kufanyika kwa usuluhisho wa taarifa katika mifumo mbalimbali na kusafisha takwimu chafu kwenye mfumo wa Epicor 10.2 ili kuwezesha kuwa na takwimu sahihi kwenye Dashboard ya mapato ya ndani;Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeendelea kushirikiana na Wadau wengine katika kuzijengea uwezo Halmashauri kukusanya mapato ya ndani ikiwemo kuzinunulia Halmashauri mashine 7,227 za kukusanya mapato na kuwajengea uwezo wataalam wa fedha katika ngazi ya Mkoa; na Ofisi ya Rais TAMISEMI imeendelea kuandaa na kusimamia matumizi ya Miongozo mbalimbali ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato.
Post a Comment