Featured

    Featured Posts

KERO YA USAFIRI DAR KUISHA JULAI MWAKA HUU, MABASI 305 YA MWENDOKASI KUANZA KAZI


Charles James, Michuzj TV

DAR kama mbele! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali kusema kwamba ifikapo Julai mwaka huu changamoto ya usafiri hasa ule wa mwendokasi itakua imekwisha jijini Dar es Salaam.

Kwa muda mrefu Jiji hilo limekua likikumbwa na kero ya usafiri kwa wananchi wake jambo ambalo limekua likikwamisha shughuli za kibiashara, wanafunzi kuchelewa mashuleni na shughuli zingine za kijamii na kiuchumi.

Sasa matumaini hayo ya kumaliza kero hiyo yametolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo wakati akielezea mafanikio ya miaka minne ya wizara hiyo.

Mhe Jafo amesema tayari washapata mzabuni mpya ambaye ataendesha mradi huo wa mwendokasi ambapo ataanza kazi ifikapo Julai mwaka huu.

Amesema mradi wa mwendokasi umekua na changamoto hasa ya uhaba wa mabasi ambayo yameshindwa kukidhi mahitaji ya wingi wa abiria wanaotumia usafiri huo.

" Kumekua na changamoto za hapa na pale kwenye mradi huu ambapo hasa ni uchache wa mabasi kwani sasa hivi yapo 140 kati ya 305 yanayohitajika.

Katika awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi ya mwendokasi, tumejifunza mazuri na mabaya ambayo yametuwezesha kuja na maboresho awamu ya pili ya utekelezaji mradi huu, changamoto zote zitabaki kuwa historia kwani mzabuni ametuhakikishia ataleta mabasi yote yanayotakiwa," Amesema Jafo.

Amesema serikali ya Rais Magufuli itaendelea kuboresha miundombinu nchini ili kuondoa adha inayowapata wananchi wake ambapo tayari awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu ya mradi huo wa mwendokasi kwenda Mbagala umekwisha aanza, lakini pia itafuatiwa na awamu ya tatu kwa ajili ya mabasi ya mwendokasi kuelekea Gongo la Mboto.

Amesema pia serikali inaendelea na maboresho ya ujenzi wa barabara za mitaa katika Jiji hilo ikiwemo kutoka Chang’ombe-Temeke mwisho hadi Sokota, Kijichi-Kibada huku mitaa 14 ikifumuliwa kwa lengo la kuimarisha miundombinu kuwa ya kisasa zaidi.

" Sisi tunatekeleza tu, niwaambie mtu alieondoka Dar es Salaam miaka mitatu iliyopita akirudi atakuta kila kona imebadilika hata kwao itabidi ashikwe mkono apelekwe maana hatopakumbuka," Amesema Jafo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala na Serikali za Mitaa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Mwanne Nchemba ameipongeza wizara hiyo kwa namna ambavyo imefanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi kwenye kila nyanja.

" Sisi sote ni mashahidi wa namna ambavyo Tamisemi imekua ikitekeleza miradi yake ambayo yote ina manufaa makubwa kwa Nchi yetu na wananchi ambao walituchagua. Niwasihi muendelee kuwatumikia watanzania kwa kasi hii hii," Amesema Mhe Mwanne.

Nae Mbunge wa Rombo (Chadema), Mhe Joseph Selasini ameipongeza Tamisemi kwa mafanikio hayo ambayo amesema yanalenga kuwainua watanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa, kidini na kikabila.

Tukio hilo la kuelezea mafanikio ya miaka minne ya wizara hiyo iliyopo chini ya Ofisi ya Rais imehudhuriwa na wakuu wa mikoa, Wilaya, wabunge, viongozi wa dini na taasisi mbalimbali za kimaendeleo ambapo Waziri Jafo alizindua kitabu kinachoelezea utekelezaji wa miradi hiyo na mafanikio yake..
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi kitabu kinachoonesha mafanikio ya Wizara yake kwa kipindi cha miaka minne katika tukio lililofanyika leo jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Tamisemi, Mhe Mwita Waitara na kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia wizara hiyo, Mhe Mwanne Nchemba.
 Wadau mbalimbali wa maendeleo wakifuatilia hotuba ya Mhe Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo wakati akielezea mafanikio ya wizara yake ndani ya kipindi cha miaka minne leo jijini Dodoma.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akielezea mafanikio ya wizara yake hiyo ndani ya kipindi cha miaka minne katika mkutano na wadau mbalimbali wa maendeleo kuelezea  hayo leo jijini Dodoma.
 Mhe Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akimkabidhi kitabu kinachoonesha miradi na mafanikio ya wizara hiyo Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana