Seneta wa ngazi ya juu nchini Pakistan sambamba na kubainisha kwamba Marekani kamwe haijawahi kuwatakia jambo la kheri Waislamu, amesema kuwa Trump hataki hata kidogo kutatuliwa matatizo ya Waislamu wa Kashmir.
Mushahid Hussain Syed ameyasema hayo wakati akizungumza na waungaji mkono wa chama cha Pakistan Muslim League (Nawaz) mjini Lahore ambapo akibainisha kuwa misimamo ya kibaguzi ya Marekani kuulenga Uislamu kamwe haitosimama, amefafanua kuwa, matarajio ya upatanishi wa Donald Trump na serikali yake katika mzozo wa Kashmir, ni ujinga mkubwa. Akiashiria mpango wa Muamala wa Karne ulio dhidi ya Palestina na kulaaniwa vikali mpango huo mchafu, ameongeza kuwa serikali ya Pakistan haifai iridhie hata kidogo upatanishi wa Trump katika mzozo wa Kashmir, kwa kuwa matokeo yake yatakuwa sawa na kadhia ya Palestina inayoshuhudiwa hivi sasa.
Seneta huyo wa ngazi ya juu wa Pakistan sambamba na kubainisha kuwa mpango wa Muamala wa Karne ni mwendelezo wa hatua za kibaguzi za Marekani kuwalenga Waislamu na kwamba rais huyo wa Marekani anakusudia kuunda Israel iliyo kubwa kupitia mpango huo, ameongeza kuwa, ni lazima serikali ya Islamabad mbali na kutoa msimamo mkali wa kuupinga utawala haramu wa Kizayuni, pia isimpe nafasi Trump ya kuweza kuingilia masuala ya ndani ya Pakistan hususan katika kadhia ya Kashmir.
Post a Comment