Na. Peter Haule na Josephine Majula, WFM, Dodoma
Serikali imeuomba Umoja wa Ulaya (EU) kuwekeza katika maeneo ya maendeleo ambayo tayari Serikali imeanza kuyatekeleza ikiwemo uboreshaji wa miundombinu katika mkataba mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na EU kwa mwaka 2021 hadi 2027.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti, kuhusu ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi.
Dkt. Mpango alisema kuwa, katika mkataba mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na EU unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2021 ni vema ukaendelea kuimarisha maeneo ya maendeleo ambayo tayari yameanza kutekelezwa na Serikali hususani katika Sekta ya Elimu, Afya, miundombinu na mingine ili kufikia malengo endelevu.
“Tuna kazi kubwa ya kuwekeza kwenye rasilimali watu kwa kuwa miradi kama miundombinu haiwezi kufikia malengo yake bila kuwa na uwekezaji katika rasilimali hiyo na ndio maana kama Serikali tumeamua kutoa elimu bure kuanzia shule ya Msingi hadi Sekondari”, alieleza Dkt. Mpango.
Alisema kuwa katika suala la miundombinu, Serikali inaangalia uwezekano wa kuanza ujenzi wa Reli kutoka Bandari ya Mtwara katika Bahari ya Hindi hadi Bandari ya Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa, ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuokoa fedha nyingi zinazotumika kukarabati barabara zinazoharibika kwa usafirishaji wa bidhaa kwa njia ya barabara.
Aidha alieleza kuwa miundombinu hiyo ya reli itakuwa na matawi kuelekea Liganga ambako kunapatikana madini ya Chuma na Mchuchuma ambako kuna hazina kubwa ya Makaa ya Mawe.
Alisema Reli hiyo itasaidia pia kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani ikiwemo Malawi, hivyo kuchochoa biashara na kuongeza mapato.
Kwa upande wake Balozi wa EU nchini Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti, aliipongeza Serikali kwa kuwa na Sera nzuri za maendeleo lakini pia akasema kuwa ili kuboresha mazingira ya kibiashara, miongoni mwa mambo yanayohitajika ni pamoja na Miundombinu, mafunzo, kuwa na uchumi wa kidigitali na siasa bora, mambo ambayo Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuyatekeleza.
Mkataba wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi uliokuwa ukitekelezwa kuanzia mwaka 2014 unamalizika mwaka huu ilihali kwa sasa kunatarajiwa kuwepo kwa majadiliano ya mkataba mwingine wa ushirikiano unatarajia kuanza kutekelezwa mwaka 2021 na kumalizika 2027.
Katika tukio jingine, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango namekutana na mkufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikianao wa Biashara wa Finland, Mhe. Ville Skinnari, ambapo walijadili mambo mbalimbali yakiwemo masuala ya ushirikiano na maendeleo ya kiuchumi.
Post a Comment