Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel zimetumia ndege ya abiria kama ngao ya kujikinga katika uvamizi wake mpya dhidi ya Syria.
Msemaji wa wizara hiyo, Meja Jenerali Igor Konashenkov alisema jana Ijumaa kuwa, ndege ya abiria ya Airbus-320 iliyokuwa na abiria 172 nusra ipigwe na makombora ya Israel ikielekea Damascus kutoka Tehran. Hata hivyo mfumo wa ngao ya makombora ya Syria mjini Damascus ulifanikiwa kutungua makombora hayo ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia ameeleza bayana kuwa, baada ya kukoswakoswa na makombora ya Wazayuni, ndege hiyo ya abiria ililazimika kutua kwa dharura katika uwanja wa kijeshi wa Hmeymim katika mkoa wa pwani wa Latakia, magharibi mwa Syria.
Meja Jenerali Konashenkov amekosoa mienendo hiyo ya Israel ya kufanya mashambulizi yake ya makombora bila kujali ndege za abiria zinazoruka katika anga ya Syria akisisitiza kuwa, kitendo hicho kinaonyesha namna Tel Aviv isivyoyapa thamani maisha ya wanadamu hususan raia ya kawaida.
Mgogoro wa Syria uliibuka mwezi Machi 2011 baada ya makundi mengi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati, Marekani, utawala haramu wa Israel na washirika wao kuivamia nchi hiyo kwa lengo la kubadili mlingano katika eneo la Asia Magharibi kwa maslahi ya utawala huo wa Kizayuni.
Hata hivyo, msimamo imara wa serikali ya Damascus chini ya uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na washirika wake, umeweza kufelisha njama hizo za maadui sambamba na kuyashinda makundi hayo ya kigaidi.
Post a Comment