Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, lina wasiwasi mkubwa na hali inayozidi kuwa mbaya katika eneo la Beni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na raia kuendelea kuyakimbia makazi yao.
Taarifa ya UNHCR imeeleza kuwa, raia katika maeneneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanazidi kuyakimbia makazi yao kutokana na kuzidi kuzorota hali ya ukosefu wa usalama katika maeneo hayo.
Ripoti ya Shirika hilo la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) inaeleza kuwa, machafuko huko Beni yamesababisha zaidi ya watu 100,000 kuyakimbia makazi yao katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Wasiwasi huo wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) unaripotiwa katika hali ambayo, idadi ya watu wanaouawa na mashambulio ya makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nayo inazidi kuongezeka.
ADF
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari, vijiji vinne katika mji wa Beni uliopo mashariki mwa nchi vilishambuliwa na wapiganaji wa kundi la ADF–Nalu wenye asili ya Uganda, ambapo raia wasiopungua 30 waliuawa kwa kuchomwa visu na kupigwa mapanga na makumi ya wengine kujeruhiwa vibaya.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo hao wa ADF wa Uganda wamekuwa wakiwashambulia raia, maafisa usalama na hata maafisa wa afya wanaopambana na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi hiyo na kuhatarisha usalama katika maeneo hayo.
Post a Comment