<<Rais Dk. John Magufuli akimpandisha cheo DCP John Masunga kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika hafla ya kuwaapisha viongozi wa Wizara, Mahakama, Majeshi na Mikoa aliowateua Januari 31, 20202, iliyofanyika leo, Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Februari 3, 2020. (Picha na Ikulu)
IKULU, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli amewaapisha viongozi wa Wizara, Mahakama, Majeshi na Mikoa katika hafla iliyofanyika leo, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao ambao Rais aliwateua Januari 31, 2020 na kuwaapisha leo nyadhifa zao zikiwa kwenye mabano ni, Zena Ahmed Said (Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati), Prof. Riziki Silas Shemdoe (Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara), Christopher Derek Kadio (Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi), Dk. Hassan Abbas Said (Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) na Mary Gasper Makondo (Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi).
Wengine ni Brigedia Jenerali Suleiman Mungiya Mzee (Kamishna Jenerali wa Magereza), John William Masunga (Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji),Stephen Muhoja Mashauri (Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma), Emmanuel Mpawe Tutuba (Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza) na Judica Haikase Omari (Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga), Leonard Robert Masanja (Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati) na Nathaniel Mathew Nhonge (Kamishna wa Ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi).
Wilbert Martin Chuma (Msajili Mkuu wa Mahakama), Kelvin David Mhina (Msajili wa Mahakama ya Rufani),
Jaji Dk. Gerald Alex Ndika, Julius Bundala Kalolo na Genoveva Namatovu Kato (Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama) na pia Rais Dk. Magufuli ameshuhudia Jaji Kiongozi Dk. Eliezer Feleshi akimuapisha Sharmillah Said Sarwatt kuwa Msajili wa Mahakama Kuu.
Taarifa ya Ikulu imesema, baada ya kuapishwa viongozi hao walikula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kiapo ambacho kilioongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela, mbele ya Rais Magufuli.
Akizungumza baada ya uapisho huo, Rais Magufuli amemtaka kila mmoja kwenda kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu, na kuchapa kazi kwa manufaa ya Watanzania wote na kutoa mwito kwa viongozi hao kwenda kushirikiana ipasavyo na viongozi wengine waliopo katika ofisi zao huku akiwataka viongozi na watendaji wa ofisi hizo kutoa ushirikiano kwa viongozi hao wapya.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa ya Tanga, Ruvuma, Mwanza na Dar es Salaam, viongozi wa Dini, viongozi wa siasa na viongozi wa taasisi mbalimbali.
Post a Comment