Mary Mwakapenda
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli atazindua Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) siku ya Jumatatu tarehe 17 Februari, 2020 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere , Dar es Salaam.
Aidha, tukio hili litashuhudiwa pia na Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) amesema tathimini ya Utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha Mpango inaonyesha kuwa Mpango huu umesaidia kufanikisha azma ya Serikali ya kupunguza umaskini nchini ambapo takwimu zinaonyesha kwamba umaskini wa mahitaji ya msingi kwa kaya za walengwa umepungua kwa asilimia 10 na umaskini uliokithiri umepungua kwa asilimia 12 kwa kaya maskini sana nchini.
Mhe. Mkuchika amesema pamoja na mafanikio hayo, walengwa waliofikiwa na sehemu ya kwanza ya Mpango wa Kunusuru kaya maskini ni asilimia 70% ya wananchi wanaoishi katika hali duni.
“Ili kuwa na maendeleo yanayogusa wananchi wote, Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kuendelea na Kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya maskini ili kaya zote zinazoishi katika mazingira duni zipate usaidizi wa TASAF kwa kuwawezesha kufanya kazi na kupambana na umaskini ikiwa pia ni moja ya agenda kuu katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015.” Mhe. Mkuchika amesisitiza.
Kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF ambacho kitazinduliwa na Mhe. Rais kitatekelezwa katika halmashauri 185 za Tanzania bara, Unguja na Pemba kwenye vijiji/mitaa/shehia zote nchini na kujumuisha maeneo ya vijiji/mitaa /shehia ambayo hayakupata fursa hiyo katika kipindi cha kwanza cha utekelezaji wake ambacho kilikamilika mwezi Disemba mwaka jana (2019).
Aidha, Kipindi hiki kitafikia Kaya milioni 1.4 zenye jumla ya watu milioni 7 kote nchini hii ikiwa ni nyongeza ya kaya laki tatu ukilinganisha na kaya zilizofikiwa katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu.
Mhe. Mkuchika amesema mkazo mkubwa katika kipindi cha pili utawekwa katika kuwezesha Kaya zitakazoandikishwa kwenye Mpango wa KUFANYA KAZI ili kuongeza kipato, pia huduma za jamii zitaongezwa na kuboreshwa ili kuendeleza rasilimali watoto hususan katika upatikanaji wa elimu na afya.
“Ni matarajio ya Serikali kupitia utekelezaji wa shughuli za TASAF katika kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu kuwa kiwango cha umaskini kitapungua na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi ukiwemo ule wa viwanda ambayo ni agenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.” Mhe. Mkuchika amesisitiza.
Mhe. Mkuchika ametoa rai kwa Watanzaia kuhakikisha wanaosajiliwa kwenye Mpango huu ni wale tu waliotimiza vigezo vilivyowekwa na sio vinginevyo ili kuepuka usumbufu.
Post a Comment