Featured

    Featured Posts

SPIKA MSTAAFU ANNE MAKINDA AWATAKA WANAWAKE KUACHA UOGA


  Spika msaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amewataka wanawake nchini kuacha uoga katika wakati wa mapambano ya kutafuta fursa mbalimbali za kielimu, uchumi na siasa vinginevyo masuala ya usawa wa kijinsia itabaki kuwa ndoto.

Makinda amesema hayo jijini DODOMA katika Kongamano la uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambalo pamoja na mambo mengine limejadili utekelezaji wa maazimio ya ulingo wa Beijing yaliyowekwa miaka 25 iliyopita.


  Amesema wanawake nchini Tanzania ni zaidi ya asilimia 51 ya wananchi wote hivyo kundi hili lina uwezo kufikia maamuzi yenye tija kwa wanawake lakini tatizo kubwa ni woga wa kuthubutu ilhali uwezo wanao.

“Wanawake acheni uoga na unyonge maana wanawake ambao ni wawakilishi wa majimbo wameendelea kuaminika na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa amesema.

Ameongeza kuwa, jitihada zinaonekana ingawa zinasuasua sana hasa kwenye mambo ya siasa.
Hatuwezi kusema tuna usawa wa kijinsia wakati bado hatujaweza kuchaguliwa na watu. Kama isingekuwa kipengele cha viti maalum, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lingekuwa na wanawake asilimia 6 tu, idadi ambayo ni ndogo sana”

Ameongeza kuwa asilimia 30 ya wabunge wa viti maalum na wale wa kuteuliwa haina mantiki katika kuelekea usawa wa kijinsia.

Amewahimiza wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi hasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020.


  Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mchango wa viongozi wanawake wakiwemo wastaafu umeleta mabadiliko makubwa katika kuelekea maendeleo jumuishi.

Waziri Mwalimu amemtaja Mama Makinda kuwa kuwa kioo kwake wakati wa kutekeleza majukumu yake katika Wizara huko akiwapongeza wanawake walioshiriki katika harakati za kuelekea ukombozi wa mwanamke maarufu kama Mkutano wa BEIJING.


  Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiwasilisha utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Beijing amesema mambo mengi yamefanyika ikiwemo kuwezesha wanawake kiuchumi kupitia mifuko ya uwezeshwaji kiuchumi.

Dkt. Jingu amesema kwa kipindi cha miaka minne, zaidi ya shilingi bilioni 39 zimetolewa kwa wanawake zaidi ya laki 8 kupitia asilimia 10 ya fedha za ndani za Halmashauri na shilingi bilioni 2 zimetolewa kwa zaidi ya wanawake elfu 3 kupitia dirisha la wanawake la Benki ya Posta Tanzania mwezi Agosti 2018 hadi Machi 2019.



Ameongeza pia kuwa, umiliki wa ardhi umeongezeka kwa wanawake kutoka asilimia 6 mwaka 2014 hadi 16 mwaka 2017 pamoja na ushiriki wa wanawake katika maonesho ya Biashara ya kimataifa kutoka 1183 mwaka 2017 hadi 13016 mwezi Machi mwaka 2019.

  Kongamano hilo  la siku moja limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wadau wa afya na wanafunzi kutoka shule za Sekondari zilizopo mkoani Dodoma.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana