Kwa mara nyingine, waandishi habari wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB World Service) wamelengwa na magaidi nchini Syria na kujeruhiwa.
Katika hujuma hiyo maroketi ya magaidi yamewalenga waandishi habari wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusini mwa Halab (Aleppo) kaskazini mwa Syria, waandishi habari wa Al Kauthar na Al Alam pamoja na wapiga picha waliokuwa wameandamana nao. Waandishi wa habari hao wamejeruhiwa wakati wakiripoti matukio katika medani ya mapambano katika vitongoji vya kusini mwa Aleppo.
Mgogoro wa Syria ulianza mwezi Machi 2011 na ikifika Machi 2020 utakuwa mwaka wa kumi wa mgogoro huo. Katika kipindi cha miaka tisa iliyopita, kuakisiwa mgogoro huo katika vyombo vya habari ni jambo ambalo limekuwa na umuhimu mkubwa. Vyombo vya habari na waandishi habari huwa na nafasi muhimu katika vita.
Joseph Nye, msomi maarufu Mmarekani anasema, vyombo vya habari vina uwezo wa kubadilisha mitazamo na kukuza au kudunisha migogoro.
Wakati wa Intifadha ya Pili mwaka 2000, kanali ya Televisheni ya Al Jazeera ilitangaza taswira za utawala haramu wa Israel kumuua shahidi Muhammad al-Durrah mtoto Mpalestina aliyekuwa na umri wa miaka 12 akiwa amekumbatiwa na baba yake. Taswira hii iliwawekea wazi walimwengu taswira ya namna utawala wa Kizayuni wa Israel ulivyokuwa ukitenda jinai.
Ingawa mgogoro wa Syria unaakisiwa na vyombo vyote vya habari duniani, lakini vyombo vya habari vya habari vya Magharibi vyenye satwa pamoja na vyombo maarufu vya habari vya nchi za Kiarabu vimekuwa vikiakisi mgogoro wa Syria kwa maslahi ya madola ya Kimagharibi na tawala vibaraka wao.

Vyombo hivyo vya habari vimekuwa vikieneza habari zilizojaa hadaa na zisizoakisi ukweli wa mambo kuhusu mgogoro wa Syria kwa lengo la kuchochea hisia za dunia dhidi ya serikali halali ya Syria.
Mbinu hii ya kueneza hadaa imebainika wazi wakati wa kuenezwa uvumi kuhusu serikali ya Syria kutumia silaha za kemikali.
Katika hali kama hiyo, vyombo huru vya habari ambavyo vimekuwa katika medani ya vita nchini Syria vimekuwa vikijaribu kueneza habari sahihi na zinazoakisi ukweli wa mambo ili kukabiliana na vyombo vya habari vya Magharibi. Vyombo vya habari vya Kitengo cha Kimataifa cha IRIB ni kati ya vyombo huru vya habari duniani ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kuakisi ukweli wa mambo Syria.
Wakati katika kazi yao hiyo, waandishi habari wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB si tu kwamba wamekuwa wakikabiliwa na hujuma ya propaganda za maadui bali pia wamepoeka vitisho kutoka kwa magaidi na hata baadhi yao wameuawa shahidi. Maya Nasser, mwandishi habari wa Press TV aliuawa shahidi baada ya kulengwa na magaidi mjini Damascus mwezi Septemba 2012.
Naye Mohsen Khazai, mwandishi habari wa IRIB mnamo Novemba 2016 aliuawa shahidi katika hujuma ya maroketi ya magaidi katika mji wa Halab nchini Syria.

Aidha Mohammad Hassan Husseini, mwandishi wa habari wa IRIB alijeruhiwa vibaya Agosti 2015 wakati akiripoti kuhusu operehseni za Jeshi la Syria katika miinuko ya Latakia kaskazini magharibi mwa Syria. Waandishi habari wengine wa Kitengo cha Kimataifa waliojeruhiwa Syria ni Dhiaa Qadru mwandishi wa Al Alam, Ibrahim Al Kahil mpiga picha wa Al Alam. Jumapili tarehe pili Februari 2020 Sahib Al Masri, mwandishi habari wa Al Kauthar naye pia alijeruhiwa magharibu mwa Halab.
Kuuawa shahidi na kujeruhiwa waandishi habari wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB ni jambo linaloonyesha kuwa wanasambaza ujumbe mkubwa na wa ukweli ambao una wasikilizaji na watazamaji wengi. Pamoja na changamoto zote hizo, harakati ya kufikisha ujumbe huu itaendelea kwa mapenzi na azma imara.
Post a Comment