TAARIFA YA KIKAO HICHO
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya yaani DCC lengo kuu likiwa ni kupata maoni na ushauri kutoka kwa wajumbe kuhusu bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi uliopo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mhe. Kisare Makori aliambatana na Katibu Tawala Ndg. James Mkumbo, Mkurugenzi wa Manispaa Beatrice Dominic na wajumbe wengine waliohudhuria ni viongozi wa vyama vya siasa, wakuu wa Idara na watendaji.
Wakati akifungua kikao hicho Mwenyekiti aliwasisitiza wajumbe kuwa lengo kuu la kikao ni kushauri katika maeneo ambayo pia wanaona yanastahili marekebisho na Wilaya itatilia mkazo na kuyafanyia kazi.
Aliongeza kuwa shughuli za vyama vya siasa zinafanywa kwa mujibu wa sheria na ndio maana viongozi wanakuwa wajumbe ili kusaidia kuleta maendeleo katika Wilaya.
"Hata Mhe. Rais amekuwa akisisitiza kuwa maendeleo hayana Chama, na ndio maana leo tuko wote hapa kwa ajili ya kumsaidia kuleta maendeleo ya Wilaya yetu” Aliongeza Mkuu wa Wilaya.
Aliwaambia pia kuwa nia nyingine ni kuhakikisha uongozi wa Halmashauri unatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Katika kuchangia Mjumbe Coaster J. Kibonde ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia Makini Wilaya ya Ubungo alisema kuwa amefurahishwa kwa namna serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli inavyotekeleza miradi ya maendeleo na wananchi wanaiona. ”Nikuombe Mhe. Mkuu wa Wilaya kwa kuwa tunaamini kuwa wewe ni msikivu, wakati wa ziara za kutembelea miradi ya maendeleo na sisi kutoka vyama vingine vya siasa tualikwe ili tukawe mashuhuda wazuri wa namna mnavyotekeleza Ilani” alisema Ndg. Coaster.
Mjumbe mwingine ambaye ni Katibu wa ACT wazalendo Ndg. Kassim Chogamawano aliiomba Halmashauri kutenga fedha ili kumalizia mradi wa machinjio Manzese pamoja na kuwa na fedha iliyotengwa kwa ajili ya machinjio ya kisasa Kibesa.
Mhe. Kisare aliwaomba wajumbe kufuata Utawala wa Sheria na kuwashukuru kwa kujitokeza kwao. Aliwasisitiza kutosubiri hadi kikao kitokee ili kujadili masuala mazima ya maendeleo kwani ofisi yake na Ofisi ya Mkurugenzi zipo wazi kwa ajili ya kusikiliza wananchi Kwa Maendeleo ya Ubungo.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO
MANISPAA YA UBUNGO
Post a Comment