Featured

    Featured Posts

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI MHE. JAJI WA RUFAA (MST) SEMISTOCLES KAIJAGE KWENYE MKUTANO WA TUME NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA MWL. NYERERE TAREHE 23 MACHI, 2020

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage akihutubia wakati wa mkutano na Viongozi wa Vyama vya Siasa jijini Dar es Salaam



Sehemu ya viongozi wa Vyama vya Siasa na wadau wengine wakisikiliza kwa makini wakati Mwenyekiti wa  NEC, Jaji Mstaafu akihutubia katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikitano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam. PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA.



           Mkurugenzi wa Uchaguzi,
           Msajili wa Vyama vya Siasa,
           Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa,
           Viongozi wa Vyama vya Siasa,
           Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu,
           Inspekta Jenerali wa Polisi,
           Kamishna Mkuu wa Uhamiaji
           Watendaji wa Tume,
           Waandishi wa Habari,
           Mabibi na Mabwana

Bwana Asifiwe!!!, Tumsifu Yesu Kristu!!!,  Assalam Aleykum!!!.

Kwanza, kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi,naomba kutumia fursa hii, kuwakaribisha katika mkutano huu muhimu ambao madhumuni yake ni kupeana taarifa na kujadiliana kwa pamoja kuhusu kukamilika kwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza. Pia, ni kuwafahamisha kuhusu maandalizi ya zoezi la uwekaji wazi wa Daftari la Awali, pamoja na kuwapa taarifa juu Maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili.

Kama mnavyofahamu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, uandikishaji wa Wapiga Kura na Uwekaji wazi wa Daftari la Awali ni masuala muhimu.

Pili, ningependa nitumie fursa hii, kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa namna ambavyo  mmetoa ushirikiano kwa Tume wakati  wote wa zoezi la Uboreshaji wa Daftari Awamu ya Kwanza. Niwaombe muendelee kutoa ushirikiano huo katika michakato inayoendelea. Tume inaamini kuwa mafanikio ya mazoezi inayoyaratibu na kuyasimamia yanatokana na ushiriki wa Wadau wa Uchaguzi hasa  ninyi wa Vyama vya Siasa.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Bila shaka mnakumbuka kuwa tarehe 13 Juni, 2019 tulikutana nanyi, hapa Dar es Salaam, kwa lengo la kupeana taarifa za kuanza kwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Awamu ya Kwanza.
Katika mkutano huo, Tume iliahidi kukutana nanyi katika hatua mbalimbali za michakato ya uchaguzi kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu wa 2020. Leo, kwa mara nyingine,. tunaendelea kutekeleza ahadi yetu hiyo.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Kama nilivyosema hapo awali mkutano wetu una mambo matatu.   Kwanza, ni kuwapa taarifa ya kukamilika kwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Awamu ya Kwanza, pili ni kuwapa taarifa yakuwepo kwa zoezi la Uwekaji wazi wa Daftari hilo,  na tatu ni kuwapa taarifa ya maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya  Pili.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Tume imekamilisha zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya kwanza nchi nzima, kwa mafanikio. Zoezi hili lilianza tarehe 18 Julai, 2019 katika Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na kukamilika 23 Februari, 2020  katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Kabla ya kuanza uboreshaji, Tume kwa kutumia taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ilifanya makadirio ya Wapiga Kura wapya watakao andikishwa. Makadirio hayo ya uandikishaji yalikuwa ni asilimia 17 ya Wapiga Kura walioandikishwa mwaka 2015 ambao ni Milioni ishirini na tatu, laki moja sitini na moja elfu, mia nne na arobaini (23,161,440) 

Uchambuzi wa taarifa za zoezi la Uboreshaji kwa Awamu ya Kwanza unaonesha kwamba, Wapiga Kura wapya walioandikishwa ni Milioni saba, arobaini na tatu elfu, mia mbili arobaini na saba (7,043,247) sawa na asilimia 30.41 ya Wapiga Kura walioandikishwa mwaka 2015. Idadi hii imezidi matarajio na makadirio ya awali kwa  asilimia 13.41.

Wapiga Kura waliojitokeza kuboresha taarifa zao ni  Milioni tatu, laki mbili, ishirini na tano elfu, mia saba na sabini na nane (3,225,778) ambayo ni sawa na asilimia 13.93 ya Wapiga Kura walioandikishwa mwaka 2015. Aidha, idadi ya Wapiga Kura Elfu kumi na sita, mia saba na saba (16,707) sawa na asilimia 0.07 ya Wapiga Kura walioandikishwa mwaka 2015, waliondolewa kwenye Daftari kwa sababu wamefariki na wengine kupoteza sifa.

Jumla ya Wapiga Kura waliopo katika Daftari la Awalikwa sasa ni Milioni thelathini, laki moja themanini na saba elfu, mia tisa  themanini na saba (30,187,987).
Idadi hii inaweza  kubadilika baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki na uchakataji wa taarifa za Wapiga Kura endapo watabainika waliojiandikisha zaidi ya mara moja.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Pamoja na mafanikio ya kukamilisha zoezi hilo kwa amani na mwitikio mkubwa wa Wapiga Kura, Tume ilikutana na changamoto mbalimbali katika kipindi hicho cha uboreshaji. Changamoto hizo ni pamoja na kuharibika kwa miundombinu katika baadhi ya maeneo, kulikotokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Hivyo, njia mbadala zilitumika kuhakikisha vifaa na watendaji wanafika katika maeneo ya uandikishaji.

Changamoto nyingine ni baadhi ya watu kutozitumia vizuri  siku  saba (7) zilizopangwa kwa ajili ya uandikishaji na kujikuta wakijitokeza siku za mwishoni na hivyo kusababisha misongamano ya watu vituoni. Hali hii ilijitokeza pia Mkoani Dar es salaam kutokana na idadi kubwa ya watu na wananchi wengi kuwa kazini siku za katikati ya wiki.  Hivyo, Tume iliongeza siku tatu (3) ili kuwapa nafasi wananchi wengi zaidi kushiriki katika zoezi hilo.
Tume itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi  juu ya umuhimu wa kujitokeza kwa wakati katika muda utakaokuwa umepangwa kwa ajili ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Hatua nyingine muhimu inayofuata baada ya kukamilika kwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni uwekaji wazi wa Daftari la Awali. Uwekaji wazi huu utafanyika, kwa mujibu wa vifungu vya 11A na 22 vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, na kifungu cha 15A cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, ambapo Tume inatakiwa kuweka wazi Daftari la Awali, ili kutoa fursa kwa wananchi kulikagua na kuhakiki taarifa zao na kufanya marekebisho pale inapohitajika.

Lengo lingine la uwekaji wazi ni kuwaondoa watakaothibitika kukosa sifa baada ya kuwekewa pingamizi.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa
Zoezi hili la uwekaji wazi wa Daftari la Awali litawahusu si tu wale walioandikishwa katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza, bali pia wapiga kura wote walioandikishwa mwaka 2015.

Katika kuhakikisha kila Mpiga Kura aliyeandikishwa anapata nafasi ya kuhakiki taarifa zake,  Tume imeweka njia tatu (3) tofauti zitakazotumika. Njia hizo ni kama zifuatazo:- 

Kwanza, ni kwa Wapiga Kura wenyewe kufika katika vituo walivyojiandikisha na kuhakiki taarifa zao katika orodha itakayokuwa imebandikwa katika vituo hivyo.




Tatu,  ni kupitia kituo cha Huduma kwa Wapiga Kura (Call centre) ambapo wananchi watapiga simu bure kupitia namba ya simu ya kituo ambayo ni 0800782100 na kupata usaidizi katika kuhakiki taarifa zao.

Tume imeweka njia zote hizo ili iwe rahisi kwa Wapiga Kura wote kuhakiki taarifa zao.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa
Daftari la Awali litabandikwa katika vituo vyote vilivyotumika kuandikisha Wapiga Kura katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza, lakini uboreshaji wa Daftari wa Awamu ya Pili na uwekaji wa Pingamizi utafanyika katika vituo vilivyoteuliwa na Tume katika kila Kata. Idadi ya Vituo hivyo nchi nzima  ni Elfu nane na thelathini na moja (8031) na leo hii mtapewa orodha ya vituo hivyo kwa njia ya nakala tepe na nakala ngumu.


Katika vituo hivyo kutakuwa na BVR Kits kwa ajili ya kufanya marekebisho husika.  Kwa hiyo, Mpiga Kura aliyehakiki taarifa zake kwa kutumia njia yoyote kati ya hizo tatu zilizotajwa na  kuhitaji kurekebisha taarifa zake, basi atakwenda kwenye kituo kilichoteuliwa kwa ajili ya zoezi hilo.


Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Tume imekamilisha  maandalizi kwa ajili ya zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili, ambapo Kwa mujibu wa Kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Tume inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara  mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na unaofuatia.
Uboreshaji wa awamu hii, kama ulivyokuwa ule wa Awamu ya Kwanza, utawahusu Wapiga Kura wapya ambao  ni raia wa Tanzania waliotimiza umri wa miaka 18 au watatimiza umri huo siku ya Uchaguzi Mkuu. Zoezi hili  pia litawahusu wale wanaoboresha taarifa zao, mathalan waliohama kutoka maeneo yao ya awali na kuhamia maeneo mengine ya kiuchaguzi, na wale ambao  kadi zao zimeharibika au kupotea.  Zoezi pia litahusisha kuwaondoa kwenye Daftari, Wapiga Kura waliofariki na wengine waliopoteza sifa kwa mujibu wa sheria.

Kimsingi, awamu hii itawahusu Wapiga Kura ambao hawakupata fursa kujiandikisha katika Awamu ya Kwanza, yaani Wapiga Kura wapya au wale waliotaka kurekebisha taarifa zao.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa
Uboreshaji wa Daftari  Awamu ya Pili ambao utaenda sambamba na Uwekaji wazi wa Daftari la Awali utafanyika  katika “routes tatu. Route  ya kwanza inatarajiwa kuanza tarehe  17 Aprili, 2020.

Katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya pili, vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa  saa 12:00 jioni kwa muda wa siku nne (4) mfululizo. 

Mwandishi Msaidizi katika kila kituo kilichoteuliwa,  atakuwa na  orodha ya vituo vyote katika Kata.  Hivyo, atakuwa na  uwezo wa  kuboresha taarifa za Mpiga Kura yeyote atakayefika kituoni kwenye Kata husika. Aidha, Mwandishi huyo atakuwa na uwezo wa kumwandikisha Mpiga Kura  kulingana na kituo atakachopigia kura siku ya Uchaguzi Mkuu  ndani ya  Kata husika.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Elimu ya Mpiga Kura ni eneo lingine muhimu katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Kama tunavyofahamu kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kimeipa Tume mamlaka  ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima,  kusimamia na kuratibu Taasisi au Asasi za kiraia zilizopewa vibali vya  kutoa Elimu hiyo.

Katika Uboreshaji huu wa awamu ya pili, Tume itaendelea kutoa Elimu ya Mpiga Kura kwa kutumia njia mbalimbali kama vile Gari la matangazo la Tume, Vyombo vya Habari, Vipeperushi na Mitandao ya Kijamii.
Aidha, vipindi mbalimbali katika redio  za kijamii vitatumika kuelimisha Umma, kutoa ufafanuzi, kujibu maswali na kupokea ushauri kutoka kwa wasikilizaji ambao ndio walengwa.

Tume pia itaendelea kutumia mitandao ya kijamii katika kuelimisha na kuhabarisha Umma hasa Vijana. Nguvu ya mitandao ya kijamii imeonekana katika  Uboreshaji wa Awamu ya Kwanza kwa namna ilivyofanikisha kuwafikia vijana na jamii kwa ujumla.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Kama ilivyo ada,  Tume hutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu. Hivyo, hata Uboreshaji wa Daftari wa awamu hii pia utasimamiwa na kuendeshwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu.
Ushauri unaotolewa kwa wadau wa uchaguzi hususan ninyi Vyama vya Siasa, ni kuendelea kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni ili awamu hii nayo, ikamilike kwa ufanisi kama ilivyokuwa Awamu ya Kwanza.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Kwa namna ya kipekee,  naomba nitoe rai  kwenu kuhakikisha kwamba mnazifikisha kwenye vyama vyenu katika ngazi za Mikoa na Wilaya taarifa mnazopata kutoka Tume katika mikutano hii au kwa njia nyingine.

Hii ni kutokana na changamoto iliyojitokeza wakati Tume inakutana na wadau wa uchaguzi mikoani, ambapo baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Siasa ngazi ya Mikoa na Wilaya  walilalamikia kutopata taarifa ya kuwepo kwa Zoezi la Uboreshaji wa Awamu ya Kwanza wala taarifa kuwa Vyama vyote vilipatiwa orodha ya vituo vya kuandikisha Wapiga Kura nchi nzima.
Pia, niwasihi muendelee kutoa taarifa zilizo sahihi, kwa wakati na kwa utaratibu mliojiwekea, ili  wananchi waweze kushiriki kikamilifu.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa
Kama mnavyofahamu, hivi sasa umezuka ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya Corona ambao umeleta taharuki Duniani kote. Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo tayari zimeathirika na ugonjwa huo.
Awali, Tume ilipanga kuweka wazi Daftari la Awali na kuanza zoezi la Uboreshaji wa Daftari Awamu ya Pili tarehe 26 Machi, 2020.  Baada ya ushauri wa Serikali kuhusu kuepuka mikusanyiko ya watu ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona, Tume ilihairisha mazoezi hayo hadi tarehe 17 Aprili, 2020. Tume pia imelazimika kukifuta kikao cha wadau kilichokuwa kifanyike kesho kwa kuwa kingehudhuriwa na idadi kubwa ya watu (zaidi ya mia hamsini (150))
Hivyo, Tume inajipanga kutekeleza jukumu la Uboreshaji wa Awamu ya Pili hali kukiwa na angalizo la kusambaa kwa virusi vya Corona. Tunahimizwa kuendelea kuchukua tahadhari kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya. Tume nayo katika kutekeleza mazoezi haya itazingatia tahadhari zote za kiafya kuhusu ugonjwa huo ili kuhakikisha washiriki wa michakato hiyo wanakuwa salama kiafya.
Tume itaendelea kufanya mashauriano na Serikali na Wataalamu wa Afya ili endapo kutakuwa na mabadiliko yoyote itatoa taarifa kwa wakati.

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa
Tume inaendelea  kuwasisitiza  wananchi  kujitokeza kwenda kuhakiki taarifa zao Daftari litakapowekwa  wazi katika maeneo yao. Aidha, wasisite kuwawekea pingamizi Wapiga Kura wasio na sifa za kuwemo kwenye Daftari ili waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa wale wenye sifa za kuandikishwa kuwa Wapiga Kura wapya na wenye kuhitaji kuboresha taarifa zao wajitokeze pia katika vituo hivyo vilivyopangwa.
Kwa kumalizia  napenda  kuwashukuru tena Viongozi wa Vyama vya Siasa kwa kuhudhuria kwa wingi katika mkutano huu. Tume inatarajia kupata mawazo mapya kutoka kwenu. Hali kadhalika, maoni na ushauri wenu mtakaotupa utaendelea  kufanyiwa kazi  katika kufanikisha mazoezi haya.

Baada ya kusema maneno haya machache, sasa naomba kutamka kwamba mkutano wetu umefunguliwa rasmi.

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana