Featured

    Featured Posts

MAJALIWA ATOA AGIZO KWA MAMENEJA WA TANROADS NCHINI

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akitoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, wakati akikagua ujenzi wa barabara ya mchepuo na kalvati jipya la zege katika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro eneo la Kiyegeya, ambapo mawasiliano katika barabara hiyo yamerejea.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, pamoja na uongozi wa Mkoa wa Morogoro na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakikagua hatua za ujenzi wa barabara ya mchepuo na kalvati jipya la zege katika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro eneo la Kiyegeya, mkoani Morogoro. Machi 10,2020.
Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Salehe Juma, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo Elius Mwakalinga, katika eneo la Kiyegeya, Wilaya Kilosa, Mkoani Morogoro
Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Rogatius Mativila akimsikiliza Mhandisi Jovan Djukic, kutoka kampuni ya CGI inayojenga kalvati jipya la zege na barabara ya mchepuo katika eneo la Kiyegeya, mkoani Morogoro.
*****************************
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, amewataka Mameneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuacha tabia ya kukaa ofisini na badala yake kufanya ukaguzi wa kina wa barabara na madaraja katika maeneo yao mara kwa mara.

Majaliwa ameyasema hayo baada ya kutembelea na kukagua hatua  za ujenzi wa barabara ya mchepuo aliyoagiza ijengwe na TANROADS mnamo tarehe 04 Machi, 2020 ili kuondokana na msongamano wa magari  yaliyokwama kwa muda wa takribani siku tano na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake.

“Nimepita mara ya pili kukagua hatua za ujenzi na nimeridhika kuona maendeleo yake  kwani barabara hii ya mchepuo imeondoa foleni kubwa iliyokuwepo”amesema  Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, amewasihi mameneja wa TANROADS kuhakikisha wanakagua vipenyo vya madaraja yote hususani ya muda mrefu kuona kama ukubwa wake unaruhusu maji kupenya kwa urahisi hasa vipindi hivi vya mvua nyingi. 

Majaliwa, ameitaka Wizara na TANROADS kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya  matengenezo zinatumika kikamilifu ili kuboresha mawasiliano katika barabara kuu na kuhakikisha zinapitika majira yote ya mwaka.

Waziri Mkuu huyo ametoa wito kwa wananchi wote nchini kuwa wavumilivu katika maeneo yaliyopata athari za mvua hasa katika barabara na madaraja wakati Serikali inafanya utaratibu wa ukarabati wa miundombinu hiyo pindi mvua zitakapokamilika.

“Tunaelewa mvua zinanyesha hivyo nawaasa watanzania kuwa watulivu wakati kazi ya ukarabati zinafanyika kwa dharura kwanza hadi hapo hizi mvua zitakapoisha”amesisitiza  Waziri Mkuu Majaliwa.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa kalvati  la zege katika eneo la Kiyegeya, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amemueleza Waziri Mkuu kuwa ujenzi wa awali waliweka makalvati ya chuma yenye urefu wa mita 12 kila moja kwa ajili ya dharura ambao uliwezesha magari kupita njia moja.

Mfugale amesema   kazi inayoendelea hivi sasa ni ya kujenga kitako  kitakachojengewa na kuunganishwa na kalvati la awali ili kuwezesha magari mawili kupita kwa pamoja. 

“Hivi sasa magari yanayotoka njia ya Morogoro wanapita katika njia ya awali na yanayotoka Dodoma wanapita njia ya mchepuo ili kuruhusu ujenzi kuendelea”amefafanua Mhandisi Mfugale.

Ameongeza kuwa kazi hiyo ya ujenzi inatarajia kumalizika baada ya wiki mbili ili magari yaweze kutumia njia ya awali wakati wanaendelea na ujenzi wa tabaka la lami.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana