Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii
UONGOZI wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA ) umesema kwamba uwepo wa tishio la virusi vya Corona (COVID-19) nchini umesababisha hofu kubwa kwa watu wenye uziwi kwani imekuwa ngumu kwao kupata maelekezo na miongozo ya Serikali pamoja na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jisinsia, Wazee na Watoto.
Umesema kuwa matangazo mengi ambayo yametolewa na Wizara ya Afya yanashindwa kuwafikia watu wenye uziwi kwani hakuna watalaam wa kutafsiri kwa alama kile kinachozungumzwa na hivyo kutojua kinachoendelea na kupata taarifa sahihi za kujikinga na ugonjwa kwa wakati.
Akizungumza leo Machi 19 mwaka 2020 jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Tungi Mwanjala amesema kuwa kundi la watu wenye uziwi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kimawasiliano kwani matangazo yanayotolewa kuhusu Corona hawapati taarifa sahihi kutokana na kutokuwepo kwa wakalimani wa kufafanua kinachozungumzwa.
Amefafanua kuwa kuna kundi la watu wachache tu wenye uziwi ambao wanatambua kinachoendelea kuhusu uwepo wa Corona nchini lakini walio wengi hawajui chochote na hivyo kuwafanya kuwa habarini zaidi kupata maambukizi.
Mwanjala ametoa ombi kwa Serikali kuweka utaratibu mzuri wa Mawasiliano kuhusu maelekezo yanayotolewa kuhusu ugonjwa huo kwa kuhakikisha kwenye matangazo yanayorushwa katika luninga yanakuwa na watu wa kutafsiri kwa alama kinachozungumzwa.
"Watu watu wenye uziwi na wasio na ni sehemu ya watanzania ambao nao wanahaki ya kupata maelekezo ya kujikinga na ugonjwa huu.Ombi letu kwa serikali na wizara ya Afya nikuangalia jinsi gani makundi yote haya yanaweza kupata taarifa sahihi ambayo itawafanya kuwa salama na kuchukuwa tahadhali ."amesema Mwanjala.
Ameongeza kutokana na uwepo wa ugonjwa huo kesho watakuwa na kikao cha Bodi ya Shirikisho hilo ambayo itakutana ili kujadili kwa kina na kisha kutoa tamko lao ambalo wanadhani litafanyiwa kazi na serikali na hatimaye wote tubaki salama .
Amefafanua zaidi kuwa yeye mwenyewe leo alimpeleka mtoto wake Hospitali na alipofika aliwakuta madaktari wamevaa maski, hivyo akajikuta akiwa kwenye wakati mgumu katika kuwasiliana kwani anatumia zaidi kuangalia mdomo na alama , hivyo kitendo cha kuvaliwa maski tayari kwao ni changamoto ya kupata mawasiliano.
Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho hilo Nicholaus Mpingwa amesema kuwa bado wanayochangamoto hasa katika eneo la tahadhari na kutoa mfano yeye anaweza kujikinga lakini akiingia kwenye daladala inaweza isiwe rahisi kutokana na msongamano wa watu.
Pia amesema kuwa hata kwenye vijiwe vya kahawa watu wanabadilishana vikombe na maji yanayotumika kuoshea vikombe hivyo nayo sio salama kwani hayatiririki. Ameongezaa bado watu wanapeana sigara na kuvuta bila kuchukua tahadhari ya Corona, hivyo bado kuna umuhimu wa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi huku akisisitiza kuwa watu wenye uziwi na wasiona wanastahili kupewa kipaumbele ya kupata taarifa.
Mpingwa ameongeza kuwa nchi ya China wao amepiga hatua katika eneo la teknolojia na ndio wamefanikiwa kukabiliana nao lakini kwa nchi kwetu kinachotakiwa ni kuendelea kuchukua tahadhari ambayo itasaidia watu kutopata maambukizi ya Corona.
Makamu Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Tungu Mwanjala akizungumza jambo kwa waandishi wa habari kuhus uwepo wa ugonjwa wa Corona nchini
Post a Comment