Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) cha Morogoro, Prof. Raphael Chibunda (wa pili kushoto), akipokea na kuonesha nakala ya Kitabu cha MAKING AFRICA WORLD'S LARGEST ECONOMY, kutoka kwa aliyepata kuwa Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa wa Morogoro ambaye pia alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania (TIC), Dkt. Clifford Katondo TANDARI (katikati). Kulia ni Mkurugenzi wa Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya Sokoine (SNAL), Prof. Mugyabuso Lwehabura na wa pili kulia ni Mwandishi wa Kitabu hicho, Bwana Derek Murusuri. Kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa SUA (Taaluma), Prof. Peter Gillah.
Na Calvine Gwabara, SUAMEDIA, Morogoro
Na Calvine Gwabara, SUAMEDIA, Morogoro
7/3/2020: Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amewashauri wanataaluma na Watanzania wengine kuona umuhimu wa kuyaandikia vitabu mawazo yao mbalimbali ambayo yatasaidia kubadili fikra na mitazamo ili kuchochea maendeleo ya Tanzania.
Wito huo ameutoa wakati akipokea Vitabu kumi vyenye thamani ya shilingi laki nne vilivyotolewa na Mwanafunzi wa SUA ambaye, alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Cliford Tandali.
Kitabu hicho kiliandikwa na Bwana Derek Murusuri kinaitwa "Making Africa World’s Largest Economy," yaani Kuifanya afrika kuwa yenye uchumi mkubwa zaidi Duniani.
Prof. Chibunda alisema kuna watu wengi wenye mawazo mazuri ambayo yanaweza kuisaidia Tanzania na afrika lakini wamebaki nayo kichwani mwao na wengine wanaandika na kuishia njiani na hivyo kuifanya jamii na Taifa kushindwa kunufaika na mawazo yao mazuri.
“Nakupongeza sana Bwana Derek Murusuri kwa kufanikiwa kuandika na kukamilisha kitabu hiki ambacho kinakwenda sasa kwa jamii kukisoma ili kuleta maendeleo ya taifa letu na Afrika kwa ujumla, na mawazo yako yataishi hata utakapoondoka duniani,’’ alisisitiza Prof. Chibunda.
Kwa upande wake Dkt. Clifford Tandali aliyetoa msaada wa vitabu hivyo 10 kwa ajili ya Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SNAL), alisema kuwa wanafunzi wa taaluma za maendeleo na ndaki ya Sayansi za jamii na insia kitawafaa sana kutokana na mawazo mazuri yaliyowekwa kwenye kitabu hicho.
Dkt. Tandali alibainisha kuwa baada ya kukisoma kitabu hicho, anakiri kuwa kinaonyesha kwa uwazi na undani namna ambavyo nchi mbalimbali duniani zimefanya na kupiga hatua kimaendeleo hasa katika matumizi ya sayansi na teknoloji na sasa wako mbali hata wale ambao tulipata uhuru pamoja nao.
“Mabara mengine yamesonga mbele kwa kuzingatia sayansi na teknolojia na ubunifu hivyo sisi kama watanzania tuna kila sababu ya kuikumbatia Sayansi, teknolojia na ubunifu ili tuweze kupiga hatua kwa haraka kama ambavyo wenzetu wamefanya’’Alisisitiza Dkt. Tandali.
Aliongeza kwa kusema kuwa SUA ndio mahali ambapo masomo ya sayansi yanafundishwa na teknolojia zinazalishwa hivyo nitoe wito kwa Serikali kuona sababu ya kutenga fungu maalumu ili matokeo ya tafiti hizo yaweze kusambazwa na kuisaidia jamii ya Watanzania hasa zile za kilimo,mifugo na uvuvi.
Nae kwa upande wake Mwandishi wa Kiitabu hicho kilichozinduliwa na Waziri Mkuu Mstafu Mhe. Mizengo Pinda, amemshukuru Katibu Tawala Mstaafu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Cliford Tandali kwa kutimiza maelekezo ya Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda aliyoyatoa wakati akizindua kitabu hicho, ya kutaka kitabu hicho kisambazwe vyuo vikuu ili vijana wengi zaidi wakisome na kufaidika na mawazo yaliyomo.
Akielezea malengo ya kuandika kitabu hicho alisema ni kuwaamsha, kuwatia chachu na kuwaaminisha vijana wa Afrika kuwa wanaweza kulifanya bara la Afrika kuweza kushindana kiuchumi na nchi za mabara mengine kwa kubadili mitazamo, kujiamini, kuchapa kazi na kutumia maliasili zilizopo kujiletea maendeleo.
Alisema kuwa mataifa mengine ya ulaya na Marekani, yanaendelea kuneemeka kwa raslimali zetu hizo hizo.
‘’Hili linawezekana kabisa kwa kuvunja kizuizi cha utamaduni kuwa hatuwezi hasa kwa vijana wetu walio kwenye vyuo vikuu na taasisi zingine katika kutumia Sayansi, teknolojia na ubunifu kama njia muhimu ya kuleta mageuzi ya uchumi, hasa katika karne ya sasa inayotegemea sana sayansi na teknolojia’’ Alisisitiza Derek Murusuri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SNAL) Prof. Mugyabuso Lwehabura akipokea vitabu hivyo kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo ameahidi kuvitunza na kuwapatia wanafunzi na watumiaji wa Maktaba hiyo kuvisoma na uhitaji ukiwa mkubwa wataongeza idadi yake ili mawazo ya mwandishi wa kitabu yatumiwe kuleta maendeleo
Post a Comment