Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam, Kisare Makori akifungua mafunzo elekezi kwa Wenyeviti na Watendaji wa Serikali za Mitaa, Watendaji wa Kata na Wakuu wa Idara katika Wilaya hiyo, leo katika Ukumbi wa Little Flower, Mbezi. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ubungo Lucas Mgonja na Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic. KWA PICHA ZAIDI ZA MAFUNZO HAYO, TAFADHALI>> BOFYA HAPA
Na Bashir Nkoromo, Ubungo
Wenyeviti na Watendaji wa Serikali za Mitaa, Watendaji wa Kata na Wakuu wa Idara katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, wamenolewa kwa kuwapewa mafunzo ya siku mbili ili kuwawezesha katika usimamizi na uendeshaji wa Mamlaka za Seriakli za mitaa.
Katika mafunzo hayo yaliyoanza leo katika Ukumbi wa Little Flowers, Kata ya Mbezi, viongozi na watendaji hao, wamenolewa kwa kwa mada motomoto kuhusu Uongozi na Utawala Bora, Uendeshaji wa vikao na mikutano katika ngaziza msingi za Mamlaka za serikali za mitaa na Sheria za Uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mada nyingine zilizotolewa kwa viongozi hao ni Muundo, Madaraka na majukumu ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Maadili wa serikali za Mitaa, Usimamizi wa ardhi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Uibuaji, Upangaji na Usimamizi wa Miradi shirikishi ya Jamii, Masuala mtambuka, Usimamizi wa Mikataba na Manunuzi, na Vyanzo na usimamizi wa Mapato katika Serikali za Mitaa.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori amesema ana matumaini kuwa uzoefu walionao viongozi na watendaji hao baada ya mafunzo hayo watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, kwa bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha usimamizi na uendeshaji wa shughuli za Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Wilaya hiyo kusema kuwa anayo matumaini kuwa watatumia uzoefu walionao kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
"Mnatakiwa kutambua kuwa mmeaminiwa kwa sababu mnao uwezo wa kuongoza wananchi katika namna ya kushiriki kwa ukamilifu katika kupanga na kufanya maamuzi yanayohusu maendeleo katika maeneo yenu ya kazi. Jambo la muhimu ni kuongoza kwa uadilifu, kujiamini, kujitambua na uwazi katika majukumu yenu. Ni vyema mkazingatia maelekezo yote yatakayotolewa na wawezeshaji ili muweze kuyafanyia kazi katika maeneo yenu.
Ili kufanikisha utendaji mzuri wa majukumu yenu, ni muhimu uwepo ushirikiano mkubwa kati ya Wenyeviti wa mitaa wote, Watendaji wa mitaa na Kata wote, na Wadau wengine wote. Hakikisheni mnafanyakazi na kuwa na ushirikiano mzuri na wa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Manispaa wakati wote mtakapokuwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo katika kazi zetu", alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka Viongozi na watendaji hao baada ya kupata mafunzo hayo nao wakatoe mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Mitaa.
Mafunzo hayo ambayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo Beatrice Domini, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ubungo Lucas Mgonja yatamalizika kesho.
Post a Comment