Featured

    Featured Posts

WAITARA AWATAKA WATANZANIA KUWA NA UZALENDO ULIOPITILIZA MAPAMBANO DHIDI YA CORONA

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara, akizungumza katika mkutano huo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.

Na Richard Mwaikenda, Ukonga.

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara, amewataka Watanzania kuwa na Uzalendo uliopitiliza katika mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Corona.

Amesema wawe makini na wageni wanaoingia nchini kupitia mipaka mbalimbali na njia za panya kwa kutoa taarifa panapohusika wanapomhisi mtu kaingia nchini isivyo halali kutoka nje ya nchi, kwani anaweza kuwa na ugonjwa huo hatari.

"Kila mtu awe na uzalendo uliopitiliza na hasa mipakani na kwenye njia za panya, toeni taarifa mara muonapo mgeni yeyote wa nje  au wa ndani, tujue wanatoka wapi na wamekuja kufanya nini, ili kuliepusha Taifa na ugonjwa huu hatari wa Corona." alisema Waitara.

Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam, alitoa maneno hayo, alipokuwa mgeni rasmi katika kikao cha Manispaa ya Ilala kukabidhi miradi ya ujenzi wa  madaraja ya Ulongoni A na B jijini Dar es Salaam hivi karibuni.Madaraja hayo yapo jimboni kwake.

Amesema kwa hali ilivyo hivi sasa wasimwamini mgeni yeyote, awe ndugu au siyo ndugu, wote watiliwe mashaka na endapo watahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo,watoe haraka taarifa panapohusika ili hatua zichukuliwe haraka kunusuru ugonjwa huo kuenea.

"Watanzania  tulibebe janga hili kwa uangalifu mkubwa, pokeeni maelekezo ya Serikali na kuyafanyia kazi, ikizingatiwa kwamba hii ni ajali ya kudumu  mpaka Mungu atakapo tunusuru,"alisisitiza Waitara.

Ametoa onyo kwa baadhi ya watanzania wanaopotosha kwa kutoa maelekezo ya kijinga na mzaha kuhusu ugonjwa huo,na kuwataka kuacha kabisa tabia hiyo, ama sivyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Amesema Kuwa, Serikali imejipanga vizuri jinsi ya kupambana na ugonjwa huo, ikiwemo Wizara ya Afya kila mara kutoa kwa umma taarifa sahihi na maelekezo mbalimbali kwani ina wigo mpana wa kukusanya taarifa.

Baada ya kumalizika kwa kikao cha makabidhiano ya miradi hiyo, Waitara alikwenda kukagua maandalizi ya ujenzi wa madaraja hayo ambapo katika Daraja la Ulongoni A, alikuta mafundi Kampuni ya Chonqging International Construction Corporation, wakiendelea kujenga kivuko cha muda kwa ajili ya kupita watembea kwa miguu, bajaji na bodaboda.

Baada kukagua alipata wasaa wa kuzungumza na wananchi wachache waliokuwepo eneo hilo, ambapo aliwatahadharisha kuhusu ugonjwa hatari wa Corona kwa kuwataka kuzingalia maelekezo yote yatolewayo na Serikali kupitia Wizara ya Afya.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana