Na Amiri Kilagalila, Njombe
Wakulima wa zao la parachichi wa kijiji cha Igongolo wilayani Njombe,wamesema licha ya kupata elimu na kufanikiwa katika kilimo hicho lakini wametoa wito kwa wataalamu wa serikali na wadau wa kilimo kuendelea kutoa elimu katika zao hilo kutokana na changamoto ya magonjwa wanayokumbana wakati wa kilimo.
Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa parachichi cha Nguvu kazi kilichopo kijiji cha Igongolo Fanuel Salingwa kwa niaba ya wakulima wa parachichi amewaeleza wataalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo TARI UYOLE walipofika katika kijiji hicho kuhalalisha ugawaji wa miche ya matunda ya kikundi hicho,kuwa kwa sasa wanasumbuliwa na gonjwa la kunyauka kwa miche midogo pamoja na miche mikubwa kuangusha matunda.
“Chanagamoto inayotusumbua sahizi wakulima ni magonjwa ya kunyauka kwenye upande wa miche midogo na miche mikubwa imekuwa ikiangusha sana parachichi hii ndio changamoto kubwa”alisema Salingwa
Pascalina Mtavangu na Anna Mgaya ni baadhi ya wakulima wa parachichi wa kutoka kikundi cha nguvu kazi wanasema kuna haja ya elimu kuendelea kutolewa pamoja na kuboreshewa zaidi soko la zao hilo ili wakulima wasikate tama.
“Kupitia zao hili tunaboresha maisha na kusomesha watoto,lakini tunaomba tuboreshewe soko ili mkulima asikate tama,na tumeona faida kubwa sana kwenye zao hili la parchichi”alisema Anna Mgaya
Ndabene Mlengera ni mratibu wa utafiti na ubunifu kutoka taasisi ya utafiti ya Tari uyole amesema kilimo hicho kimekuwa na manufaa makubwa kwa sasa kwa wakulima,huku akiwataka wakulima kutokukata tama na changamoto ya magonjwa sasa badala yake wafuate ushauri wa wataalamu unaotolewa.
“Kwa changamoto kama za magonjwa ni vitu vya kawaida lakini kwa mwaka huu hata mazao mengine kama mahindi na maharage unyevu umekuwa mwingi sana kwenye udogo,kwa mmea kama huu wa parachichi ni changamoto ndogo ambayo ukiinulia kipindi cha mvua inamaana yale maji badala ya kwenda chini na kuozesha mizizi yataenda pembeni na kusaidia ule mmea kutoshambuliwa na magonjwa kama wanavyodai sasa kushambuliwa”alisema Mlengera
Elitha Mligo ni afisa kilimo umwagiliaji na ushirika kutoka halmashauri ya wilaya ya Njombe,amesema ni lazima waendeleze ushirikiano kati ya serikali na wadau binafsi ili kukuza kilimo ndani ya wilaya hiyo.
“Halmashauri inashirikiana na wadau zaidi ya 40 katika nyanya mbali mbali na hasa kwa upande wa kilimo,na wenzetu wa Tari Uyole walileta aina mbali mbali za parachichi ili wakulima waweze kuchagua ni aina gani wanaipenda japo kwenye soko aina ya hasi imeshika kasi,na wakulima kwa kweli wanapenda kuendelea kujifunza ndio maana hata wengine wanatoa maeneo kwa ajili ya kuweka miche ya utafiti”alisema Elitha Mligo
Mkurugezni wa kituo cha utafiti Uyole Dkt.Tulole Bucheyeki wakati akihalalisha ugawaji wa miche ya parachichi kwa kikundi cha Nguvu kazi amewasisitiza wakulima kuto kukata tama katika kilimo hicho kwa kuwa soko lake ni kubwa duniani.
“Kwanza parachichi soko lake la kwanza ni wananchi wenyewe,wakati huo dunia nzima inahitaji parachichi na ukila soko lake ni dawa tena ni lishe,niwaombe wananchi tulime sana kwasababu soko lipo na wanunuzi wapo”alisema Bucheyeki
Kituo cha utafiti wa kilimo Tari Uyole kwa kushirikiana na halmashauri pamoja na kikundi cha Nguvu kazi,wameanzisha na kupanda miche zaidi ya 4500 ya parachichi aina mbali mbali ikiwemo hasi katika kijiji cha Igongolo,ambayo itawanufaisha wakulima 34 wa kikundi hicho kwa kupanda miche isiyopungua 132 kwa utoshelevu wa karibu ekari 2 kwa msimu huu wakilimo.
Baadhi ya miche ya kikundi cha Nguvu kazi kilichopo kijiji cha Igongolo inayoandaliwa na wanakikundi kwa kushirikiana na halmashauri na tari Uyole ili kuwasaidia wakulima.
Mkurugezni wa kituo cha utafiti Uyole Dkt.Tulole Bucheyeki wakati akihalalisha ugawaji wa miche ya parachichi kwa kikundi cha Nguvu kazi ili tayari kwa kupelekwa shamabani.
Mratibu wa utafiti na ubunifu kutoka taasisi ya utafiti ya Tari Uyole, Ndabene Mlengera akieleza jambo kuhusu kilimo cha parachichi na faida zake.
Afisa kilimo umwagiliaji na ushirika kutoka halmashauri ya wilaya ya Njombe, Elitha Mligo akieleza ushirikiano uliopo baina ya halmashauri, wakulima pamoja na kituo cha utafiti katika zao la parachichi.
Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa parachichi cha Nguvu kazi kilichopo kijiji cha Igongolo Fanuel Salingwa kwa niaba ya wakulima wa parachichi akiwa amekabidhiwa mche wa pachichi na mmkurugenzi wa kituo cha utafiti Uyole.
Baadhi ya wakulima wa parachichi pamoja na wataalamu wakiwa kwenye shamba la mfano la matunda ya parachichi
Post a Comment