Katika kutekeleza majukumu ya Wizara ya Madini kwa Mwaka 2020/2021, Bunge limeridhia na kupitisha makadirio ya Jumla ya shilingi 62,781,586,000 kwa ajili ya Matumizi ya Wizara na Taasisi zake.
Akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma April 21 ,2020 hotuba ya Makadirio Ya Mapato na Matumizi Ya Fedha Kwa Mwaka 2020/2021 Waziri wa Madini Mhe.Doto Mashaka Biteko alisema Mchanganuo wa Bajeti hiyo ni kama ifuatavyo:-
(i)Bajeti ya Maendeleo ni shilingi 8,500,000,000. ambazo zote ni fedha za ndani; na (ii)Bajeti ya Matumizi ya Kawaida ni shilingi 54,281,586,000. ambapo shilingi 21,045,927,000. ni kwa ajili ya Mishahara na shilingi 33,235,659,000 ni Matumizi Mengineyo (OC).
Aidha Waziri Biteko alisema katika Mwaka 2020/2021, Wizara inapanga kukusanya jumla ya shilingi 547,735,863,597 ikilinganishwa na shilingi 476,380,613,492 kwa mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 14.98.
Kati ya fedha zitakazokusanywa, shilingi 526,722,547,000 sawa na asilimia 96.16 zitawasilishwa Hazina na shilingi 21,013,316,597 sawa na asilimia 84 85 3.84 zitatumika na Taasisi zilizo chini ya Wizara.
Katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini Waziri Biteko alisema Wizara itaendelea kutenga maeneo yanayofaa kwa Wachimbaji Wadogo; kuwapa elimu kuhusu uwepo na faida za kuuza madini yao katika masoko yaliyoanzishwa; kutoa huduma nafuu za kitaalam kwa Wachimbaji Wadogo ikiwa ni pamoja na kuwafahamisha kuhusu uwepo wa mashapo katika maeneo yaliyobainishwa na kutengwa kwa ajili yao; na kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini yenye tija na namna ya kupata mikopo kutoka kwenye Taasisi za fedha.
Waziri Biteko aliendelea kufafanua kuwa Kwa kipindi kinachoanzia mwezi Julai, 2019 hadi Februari, 2020 jumla ya kilo 25,435.12 za dhahabu zenye thamani ya shilingi 2,772,331,030,317.99 zilizalishwa na kusafirishwa nje ya nchi kutoka katika Migodi Mikubwa na ya Kati.
Migodi hiyo ni pamoja na Geita Gold Mine, North Mara Gold Mine, Pangea Minerals (Buzwagi Mine), Bulyanhulu Gold Mine, Shanta Mine (New Luika), STAMIGOLD Company (Biharamulo Mine) na Busolwa Gold Mine (Tanzania).
Aidha, katika kipindi hicho kilo 10,102.43 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi 975,430,320,903.97 zilizalishwa na wachimbaji wadogo wa madini.
Kuhusu ujenzi wa ukuta wa Mererani Waziri Biteko alisema umesababisha kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali kwa takribani mara 13 ya kiwango kilichokuwa kikikusanywa awali ambapo katika mwaka 2019 makusanyo yaliongezeka na kufikia shilingi 2,150,000,000 ikilinganishwa na shilingi 166,094,043 zilizokusanywa mwaka 2017 kabla ya ujenzi wa ukuta huo.
Akiwasilisha Taarifa Ya Kamati Ya Kudumu Ya Bunge Ya Nishati Na Madini Kuhusu Utekelezaji Wa Majukumu Ya Wizara Ya Madini (Fungu 100) Kwa Mwaka Wa Fedha 2019/2020 Pamoja Na Maoni Ya Kamati Kuhusu Makadirio Ya Mapato na Matumizi Kwa Mwaka Wa Fedha 2020/2021 Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe.Dunstan Luka Kitandula alisema kwakuwa Wizara bado haijapata Fedha za maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge Shilingi 7,039,810,200.00 kutoka hazina hivyo Kamati inasisitiza kuwa Serikali ihakikishe kabla ya kwisha kwa mwaka wa Fedha 2019/2020, maombi ya Fedha ambayo yamepokelewa Hazina yawasilishwe kwa Wizara ili Wizara iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake.
Akiwasilisha maoni ya kambi Rasmi ya Upinzani Naibu Msemaji Mkuu kambi Rasmi yaUpinzani katika Wizara ya Madini Mhe.Joseph Haule amesema kuna umuhimu wa kupitia upya muundo wa Wizara ya Madini na kufanya marekebisho katika idara ama taasisi zenye Majukumu yanayofanana ili kuondoa gharama zisizohitajika .
Pia Kambi hiyo ya Upinzani imeishauri Serikali kuwaambia Watanzania hatima ya majadiliano ya ACACIA na fedha ambazo ilitakiwa kulipwa kama zilishalipwa kwa sababu ni jambo la umma watanzania walishirikishwa tangu Mwanzo.
Post a Comment