Mwandishi wa habari na mtunzi wa vitabu maarufu nchini Kenya, Profesa Ken Walibora amefariki dunia.
Prof Walibora aligongwa na gari katika barabara ya Landhies, jijini Nairobi Ijumaa na mwili wake umekuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa ya Kenyatta (KNH).
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, Walibora hakuonekana tangu Ijumaa na familia yake ilikuwa ikimtafuta kwa siku kadhaa kabla ya kubaini kwamba alikuwa amegongwa na gari.
Walibora ni mmoja wa watunzi mashuhuri wa vitabu nchini Kenya akiwa ameandika takribani vitabu 40.
Baadhi ya vitabu vyake maarufu ni pamoja na Siku Njema ambacho kilitumika kama kitabu cha kiada katika elimu ya sekondari nchini Kenya, na kitabu cha Ndoto ya Amerika.
Kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya uandishi na kwa watetezi wa lugha ya Kiswahili. Ingawa anakumbukwa sana kama mwandishi wa vitabu, amekuwa pia mtangazaji, mwandishi na msomi wa lugha ya Kiswahili.
Rais Kenyatta ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu.
Amemsifu Prof Walibora kama mtangazaji na mwandishi vitabu aliyebobea na ambaye kazi zake za fasihi zitaendelea kuhamasisha vizazi na vizazi.
Post a Comment