Featured

    Featured Posts

RAIS DK. MAGUFULI: SERIKALI HAITAWAFUNGIA WANANCHI MAJUMBANI WALA KULIFUNGA JIJI LA DAR ES SALAAM KWA SABABU YA CORONA, ASISITIZA WATU KUENDELEA KUCHUKUA TAHADHARI ZAIDI HUKU WAKICHAPA KAZI

Rais Dk. Magufuli akizungumza leo
KULU, Chato.
Rais Dk. John Magufuli amesema Serikali haitawafungia wananchi majumbani (lockdown) wala kulifunga Jiji la Dar es Salaam ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kuwakumba wananchi na kuathiri uchumi wa nchi, na ametaka Watanzania kuondoa hofu, kuendelea kuchukua tahadhari huku wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji mali na ujenzi wa Taifa.

“Tuwaondoe hofu wananchi, sio ugonjwa huu pekee unaosababisha vifo kwa wananchi, na sio kila anayepoteza maisha hivi sasa basi amekufa kwa Corona, nimejulishwa takwimu za mpaka jana idadi ya walioambukizwa ni 284 na kati yao takribani 100 wamepona, tuwaambie wananchi kuhusu taarifa hizi badala ya kuwaacha wanajawa na hofu hali inayoleta madhara zaidi” amesema Rais Magufuli.

Rais  Dk. Magufuli amesema hayo leo Aprili 22, 2020 wakati akizungumza na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama akiwa Chato Mkoani Geita kuhusu hali ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Rais Magufuli amewapongeza Madaktari na Wauguzi walio mstari wa mbele katika kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa Corona na ametoa mwito kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha inachukua tahadhari za kutosha kwa misaada ya vifaa vya uchunguzi wa Corona na vifaa vya kujikinga kuambukizwa au kuambukiza (barakoa) hasa baada ya baadhi yake kuhofiwa kusababisha maambukizi ya ugonjwa huo.

Rais Magufuli amewashukuru Watanzania kwa kuitikia mwito wa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona, na pia kushiriki katika siku 3 za kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe janga la ugonjwa huo.

Pia ametoa mwito kwa wenye viwanda hapa nchini kuzalisha barakoa kwa ajili ya Watanzania na vifaa vingine vya kukabiliana na ugonjwa huo yakiwemo mavazi ya watoa huduma na mashine za kupumulia kwa wagonjwa badala ya kutegemea vifaa hivyo kutoka nje ya nchi pekee.

Rais Magufuli amewataka viongozi kujihadhari na baadhi ya njia zinazotumika kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwemo kupulizia mitaa na majengo kwa kutumia kemikali zisizokuwa na uwezo wa kuua virusi vya Corona kama ilivyofanyika kwa baadhi ya Mikoa hapa nchini, na badala yake amewataka viongozi hao kusisitiza njia za uhakika za kujikinga na ugonjwa huo.

Amewataka Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaosababisha hofu kwa wananchi na kusambaza taarifa zisizo sahihi wakiwemo Wanasiasa ambao amewaonya kuacha kutafuta umaarufu wa kisiasa kupitia janga hili, na badala yake Watanzania wote waungane kupambana nalo.

Rais Magufuli ametoa mwito kwa nchi zote za Afrika kuungana kuziomba taasisi za kifedha za kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia ambazo zimetangaza kusaidia Mataifa ya Afrika, kutoa msamaha wa madeni badala ya kutaka kukopesha mikopo mingine ilihali nchi hizo zinakabiliwa na madeni ya mikopo ya zamani.

Amewatakia Waislamu wote mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao unatarajiwa kuanza siku chache zijazo na ametoa mwito kwao kutumia mfungo huo kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe janga la ugonjwa wa Corona.

Mapema kabla ya kikao hicho, Rais Magufuli amemuapisha Prof. Mabula Daudi Mchembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Prof. Mchembe amechukua nafasi ya Dkt. Zainab Abdi Seraphin Chaula ambaye amehamishwa na kuwa Katibu Mkuu wa Mawasiliano.

Rais Magufuli amesema amefanya mabadiliko hayo ili kuongeza kasi ya utendaji katika Wizara ya Afya ikiwemo kukabiliana na ugonjwa wa Corona.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana