Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza na Menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya Juu (hawapo pichani)wakati alipofanya ziara Leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu Abdul-Razaq Badru akizungumza wakati Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alipofanya ziara katika ofisi zao zilizopo eneo la Tazara jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu Abdul-Razaq Badru akimuonesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako maeneo mengine ya ofisi za Bodi wakati alipofanya ziara katika ofisi zao zilizopo eneo la Tazara jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya Juu wakimsikiliza Waziri qa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) alipofanya ziara kwenye Bodi hiyo.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekagua ofisi mpya za Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu zilizopo eneo la Tazara jijini Dar es Salaam na kuitaka Bodi hiyo kujiandaa kulipa wanafunzi wakati wowote vyuo vitakapofunguliwa.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Mei 18, 2020) baada ya kukagua ofisi hizo na kufanya kikoa cha pamoja na menejimenti ya Bodi hiyo.
”Katika kipindi hiki ambapo vyuo vya elimu ya juu vimefungwa, HESLB ihakikishe inatumia muda huu kufanyia kazi changamoto zote za wanafunzi ili vyuo vitakapofunguliwa malipo ya mikopo ya wanafunzi yafanyike kwa wakati,” amesema Waziri Ndalichako
Kiongozi huyo ameipongeza HESLB kwa kutekeleza agizo la Serikali la Kuhakikisha Taasisi zote za umma zinahamia kwenye majengo ya Serikali ili kupunguza gharama.
“Ninaamini hapa mtafanya kazi kwa utulivu na kutaongeza ufanisi katika kazi,” amesema Waziri Ndalichako.
Prof. Ndalichako pia alitumia kikao hicho kuwakumbusha watumishi wa HESLB kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Akiongea katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema HESLB ipo tayari kuwahudumia wanafunzi muda wowote vyuo vitakapofunguliwa kwa kuwa fedha zinazohitajika, mifumo na taarifa za wanafunzi zipo.
Badru ameongeza kuwa taasisi yake inakamilisha mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa kushirikisha wadau wakiwemo wanafunzi kupitia shirikisho lao, TAHLISO.
Kuhusu urejeshaji wa mikopo iliyoiva, Badru amesema TZS 160 bilioni zimekusanywa katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, Julai 2019 hadi Aprili 2020.
HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 ili kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi watanzania wasio na uwezo na pia kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.
Post a Comment